KAZI YA UTENDAJI KWENYE UJENZI INAFANYWA NA SITE FOREMAN(MSIMAMIZI WA UJENZI) KWA MIONGOZO KUTOKA KWA MSHAURI WA KITAALAMU.

Kumekuwa na sintofahamu kubwa juu ya ni nani anapaswa kuonekana katika eneo la ujenzi wakati wote akisimamia kazi kitu ambacho kimepelekea hata wateja na wamiliki wa mradi kutoelewa kinachoendelea na hivyo kufanya maamuzi yasiyo sahihi juu ya uendeshaji wa miradi yao. Takriban miezi minne iliyopita nilikubali kuwa msimamizi wa moja kati ya miradi mbalimbali ya ujenzi tunayoifanya au kuisimamia, lakini mradi huu nilijikuta nachukua jukumu kubwa zaidi ya lile nililokubaliana na mteja mwenyewe. Mteja yeye aliamua kufanya kazi yake na msimamizi wake ambaye ndiye (site foreman) ambaye atapokea miongozi kutoka ofisini kwetu.

Kilichotokea sasa ni kila aina ya maamuzi ya kiufundi na kitaalamu yaliyokuwa yanafanyika yaliletwa kwetu na waliokuwa wanaendelea na kazi tupate kuamua, na hivyo tukawa sasa ndio wasimamizi wakuu tena wa mradi huo. Hapa sasa ndipo tunaweza kupata picha ya msimamizi wa eneo la ujenzi (site foreman) ni nani. Katika mradi wowote wa ujenzi wanaoujenga au kutoa miongozo ya mradi huo ni wale washauri wa kitaalamu waliofanya kazi ya kubuni jengo na mihimili yake pamoja na kutengeneza michoro ya ramani, wale ndio wanaojua namna jengo linavyopaswa kuwa na vile linavyopaswa kufanyika.

Sasa msimamizi anayekuwepo katika eneo la ujenzi maarufu zaidi kama “Site Foreman” kazi yake kubwa ni utendaji ikiwa zaidi ni usimamizi wa mafundi na wafanyakazi wengine katika ujenzi akipokea miongozi kutoka kwa washauri wa kitaalamu waliofanya kazi ya ubunifu wa jengo la mihimili yake na kutengeneza michoro ya ramani. Msimamizi wa ujenzi katika eneo la ujenzi “Site Foreman” ambaye anaweza kuwa anaiwakilisha kampuni ya ukandarasi inayojenga au anasimama mwenyewe kama fundi mkuu ndiye msimamizi mkuu wa wakati wote wa shughuli zote za ujenzi katika eneo la ujenzi akipokea miongozi aidha kutoka kwa washauri wa kitaalamu pekee kama anajiwakilisha mwenyewe au washauri wa kitaalamu pamoja na miongozi ya kampuni anayoiwakilisha ikiwa anaiwakilisha kampuni.

Wasimamizi hawa wa eneo la ujenzi maarufu kama “Site Foremen” huwa na uwezo tofauti tofauti kadiri ya vipaji walivyojaliwa hivyo baadhi huweza kujenga uwezo mkubwa sana katika ujenzi kutokana na ule uzoefu wa kushinda kila siku na mafundi katika eneo la ujenzi wakitoa maelekezo na hivyo hufika mahali na kujenga uwezo mkubwa kuzidi hata washauri wa kitaalamu katika utekelezaji wa kazi za ujenzi. Hivyo wasimamizi hawa huonekana kama ndio wataalamu wenyewe na hata wateja kufikia mahali wakaamini zaidi na kuwaondoa wataalamu na kuwapa kazi.

Suala la kuwaamini wasimamizi hawa au watendaji wa ujenzi katika eneo la ujenzi ni sahihi kabisa na halina tatizo lolote ikiwa wanachokwenda kufanya ni utekelezaji wa mradi wa ujenzi pekee, tatizo litakuja kutokea pale ambapo watapaswa kufanya maamuzi ambayo ni ya kitaalamu nje ya kazi za ufundi au utekelezaji wa utendaji katika ujenzi. Ikumbukwe kwamba wasimamizi hawa ni watendaji katika ujenzi na wanaweza kuwa na uwezo mkubwa sana katika ujenzi na hata baadhi ya maamuzi wanaweza kuyafanya kwa kutumia uzoefu au mazoea baada ya kuona namna yanafanya na wahandisi na wasanifu kila siku lakini kuna maamuzi mengi ya kitaalamu ambayo hawana uwezo wa kuyafanya kipekee kwa kuwa wanakosa ile taaluma husika na makosa hayo yatakuja kuonekana wazi siku chache mbeleni.

Hivyo ni muhimu sana kufahamu hili wakati ambao unajaribu kufikiri kwa kawaida kwamba msimamizi wa ujenzi anaweza kuwa ndiye mtaalam na kuchukua nafasi ya kuongoza kila kitu katika eneo la ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *