GHARAMA ZA AWALI KWENYE UJENZI (PRELIMINARIES COSTS)

Gharama za ujenzi zilizozoeleka zimegawanyika katika makundi makuu mawili ambapo kuna gharama za vifaa vinavyokwenda kutumika kwenye ujenzi(materials cost) kisha kuna gharama za ufundi unaokwenda kufanyika kwenye ujenzi huo(labour cost). Mara nyingi gharama za usimamizi katika ujenzi huo huingia kwenye gharama za ufundi ikiwa msimamizi ndiye aliyewaajiri mafundi. Lakini hata hivyo kuna gharama nyingine huwa haziongelewi lakini ni muhimu sana na siku zote huhusika kwenye ujenzi ambazo ni gharama za awali katika ujenzi(prelimanaries cost) na gharama za dharura(contingency). Gharama za awali hizi huwa ni za lazima lakini gharama za dharura sio mara zote hutumika.

Sasa leo tunazungumzia gharama hizi za awali ambazo huwa zinatokea mara zote lakini hazizungumziwi sana wakati wa kupanga na kujadili gharama za ujenzi kwani huchukua sehemu fulani ya gharama za ujenzi. Gharama za awali zinazojulikana zaidi kama (preliminaries costs au mobilization costs) ni zile gharama ambazo haziingii kwenye shughuli za ujenzi moja kwa moja lakini ni sehemu ya kuwezesha mradi wa ujenzi kufanyika. Gharama za awali zinajumuisha; gharama zote za huduma katika eneo la ujenzi kama vile maji na umeme n.k., gharama za kukosi vyombo na mashine zote zitakazotumika kwenye kazi ya ujenzi, gharama za kufuatilia vibali vya ujenzi na kuviweka eneo la ujenzi, gharama za mawasiliano katika eneo la ujenzi, gharama za kusafirisha rasilimali zote zinazohusika kwenye mradi wa ujenzi kama vile mafundi, vifaa na wataalamu wanaofanya kazi katika mradi wa ujenzi pamoja na malazi yao.

Gharama za awali pia ndizo zitakazohusika katika ujenzi wa majengo ya muda mfupi yanayotegemewa kuwezesha mradi wa ujenzi kuendelea kama vile stoo ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi katika eneo la ujenzi, ujenzi wa ofisi ndogo itakayokuwepo katika eneo la ujenzi, eneo la maliwato ya wafanyakazi watakaokuwa wanafanya kazi katika eneo la ujenzi pamoja na gharama za ulinzi katika eneo la ujenzi. Ikumbukwe kwamba gharama hizi za awali hazijumuishi gharama za dharura zilizojitokeza wakati ujenzi unaendelea lakini mwanzoni hazikuonekana zinazojulikana zaidi kama (Contingency) kama vile kukutana na mwamba mgumu ambao utahitaji gharama za nyongeza kukabiliana nao au mbadiliko ya ghafla ya hali ya hewa au matukio ya asili ambayo hayakuweza kutabiriwa mwanzoni. Gharama za awali ni gharama ambazo hujulikana tangu mwanzoni na hujumuishwa kwenye gharama hizi za ujenzi. Kuweza kufahamu gharama hizi itakusaidia kama mteja au mkandarasi kuweza kuzipangilia na kujua namna ya kuzikabili kulingana na namna uliyochagua kuendesha mradi wako.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *