TUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI KUONGEZA THAMANI YA MRADI WAKO.

Moja kati ya sababu kubwa ya watu wengi kutopiga hatua kubwa kwenye maisha yao inatokana na watu kufanya mambo kwa mazoea na kufuata maneno na mazoea yaliyopo mtaani badala ya kukaa na kufikiri kwa utofauti. Mara nyingi kwenye maisha huwa tunakuja kugundua kwamba tulifanya makosa kwa kuchelewa sana wakati tukiwa tayari tumeshapoteza. Hili linachangiwa na ukweli kwamba binadamu huwa tunatumia zaidi hisia kwenye kuamua mambo badala ya kufikiri kwa kina juu ya madhara na faida ya kitu kwa muda mrefu. Hisia huteletea tamaa kubwa ya kupata vitu haraka na kwa ukubwa au maumivu yanayotuletea kukwepa kufanya maamuzi sahihi kwa kukwepa hisia za maumivu ya muda mfupi ambayo hayapo hata kiuhalisia.

Kukwepa kutumia wataalamu katika ujenzi kwa kuogopa kwamba wanaweza kuwa na gharama kubwa bila kuangalia thamani wanayoongeza na hasara kubwa ya mbeleni wanayoikwepesha ni kujaribu kutoroka maumivu ya kihisia ya muda mfupi kwa gharama ya maumivu yasiyo sahihi ya muda mrefu. Lakini kwa mtu anayefikiria kwa umakini na usahihi anaweza kuona wazi kwamba thamani inayoongezwa na hasara inayoepushwa ni kubwa sana kulinganisha na kiwango kidogo cha gharama kinachoongezeka kwa kuwatumia wataalamu. Kwa mfano kuna mradi tulikuwa tunafanya Mbeya mjini ambapo msimamizi mtaalamu alisafiri kwa muda wa wiki tatu pekee akawaachia wasimamizi wa ujenzi mradi waendelee yeye akiwa hayupo.

Aliporudi kwenye mradi alikuta makosa mengi kiasi kwamba alijilaumu kwa nini hakuwasisitiza kumpigia simu ikiwa kuna changamoto au sintofahamu yoyote kwenye michoro sambamba na kumpigia picha za kila siku za maendeleo ya mradi. Kwa kufanya hivyo tu peke yake ingeokoa gharama kubwa sana za hasara iliyoingiwa kutokana na makosa hayo na muda ambao unatumika kuvunja na kurudia tena kazi katika kuifanyia marekebisho. Hivyo kwa vyovyote vile kutumia wataalamu kwenye ujenzi kunaongeza sana thamani ya jengo lako sambamba na kukuokolea mud ana gharama ambazo ungeingia kutokana na makosa yaliyotokana na kukosekana kwa utaalamu.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp +255 717 452 790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *