HIVI NDIVYO WATU WAKO WA KARIBU WANAVYOKUIBIA KWENYE UJENZI.
Kwa sasa ni jambo ambalo liko wazi kabisa kwa kila mtu kwamba suala la wizi kwenye miradi ya ujenzi ni utamaduni uliokomaa na kuota mizizi kabisa hasa kwa mafundi wa mitaani. Yaani kuiba imekuwa ni sehemu ya mbinu ambazo mafundi wameshazihalalisha kabisa kwao kama njia ya kujipatia kipato na kwa wale wasiofanya hivyo ndio huonekana labda wana matatizo. Hii ni tabia na utamaduni wa hovyo sana lakini kwa bahati mbaya ni jambo ambalo ni vigumu sana kulikwepa ikiwa huna mikakati mikubwa na ambayo imezingatia kudhibiti kila njia na mbinu ambayo mafundi na wadau wengine huitumia katika namna ya kuiba katika maeneo ya ujenzi.
Baadhi ya watu katika kutatua hili wamekuwa wakiamua kuchukua mtu wao wa karibu ambao aidha wanamwamini kwa sababu ya ukaribu wao au wameletewa na kuaminishwa na watu wengine kwamba ni mtu mwaminifu. Hivyo humwamini na kumkabidhi jukumu la kuhakikisha vifaa vya ujenzi haviibiwi na yeye ndiye anayelinda site wakati wote. Kwa bahati mbaya sana kwao hili mbinu hii nayo kwa sehemu kubwa huwa haina mafanikio tofauti na hiyo ya kuwakabidhi mafundi moja kwa moja kwani binadamu ni wale wale na zaidi wanaambukizana tabia.
Ambacho hutokea ni kwamba mtu huyo wa karibu aliyeaminiwa kwanza mara nyingi naye huwa hana shughuli ya maana ya kufanya ndio maana unaweza kupata muda wake kiurahisi. Kwa sababu hana kazi ya kufanya basi hata kipato chake huwa ni cha kusuasua huku akiwa na mahitaji yake mengi kama binadamu wengine hivyo huwa ni rahisi kushawishiwa kuingia tamaa na kujiingiza kwenye wizi kama wote waliomzunguka anaowasimamia. Mtu huyu wa karibu aliyeaminiwa taratibu huanza kujenga mazoea na urafiki na wale anaowasimamia ambapo haanza kupiga hadithi mbalimbali za matukio ya wizi na udanganyifu ambayo yalishatokea na kuwanufaisha sana watu hivyo na yeye moja kwa moja hushawishika kufanya kama hao wengine ili naye anufaika kama hao wengine aliohadithiwa.
Baada ya hapo wanaofanya kazi hushirikiana na anayelinda vifaa visiibiwe sasa na kukubaliana ni namna gani na muda gani wataiba na wapi watapelekea na namna watakavyogawana kile walichoiba. Baada ya hapo kazi huwa rahisi sana kwa sababu yule uliyemwamini ataendelea kukuletea taarifa nzuri tu ambazo utaziamini iwe unafahamu au hufahamu chochote, hivyo utaishia kuibiwa lakini huenda hata usijue. Hii huwa haijalishi huyo anayeiba ni mtu wa karibu kiasi gani kwa sababu anaweza kuwa ni ndugu yako, rafiki yako mkubwa au hata mtoto wako, mjukuu wako au hata mzazi wako. Katika kazi ambazo tumekuwa tunafanya tumeshuhudia mpaka mzazi akimwibia mtoto na mjukuu akimwibia babu yake, yaani hata mweza wako kama hamjakaa sawa sawa naye anayeweza kuwa anakuibia achilia mbali mtu uliyeletewa na kuambiwa ni mwaminifu.
Sasa suluhisho la kuepuka kuibiwa ni lile lile ambalo tumekuwa tukielimisha na kusisitiza siku zote, kwani hilo halikusaidii tu kuepuka kuibiwa peke yake bali litakuwa na msaada sana mpaka kwenye ubora, uzuri na uimara wa jengo lako.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!