UTAMJUA FUNDI WA UJENZI KWA KUMKUTANISHA NA MTAALAMU MSANIFU AU MHANDISI.

Moja kati ya makosa makubwa yamekuwa yakifanywa na watu wanaofanya miradi yao ya ujenzi ni pamoja na kuamini watu wanaokwenda kufanya miradi yao ya ujenzi bila kuwathibitishia kwamba ni watu sahihi wa kuendesha miradi hiyo ya ujenzi. Hili limekuwa likipelekea watu kuumizwa sana na watu hao kwa namna mbalimbali kuanzia kutokuwa ni watu wenye ujuzi sahihi au kuwa ni watu wasio waaminifu kwa maana ya wezi na wadanganyifu. Hata hivyo hili limekuwa ni gumu kwa wengi kwa sababu kwanza wanakuwa wamewaamini kutokana na njia walizotumia kuwapata lakini pia ni ngumu mtu kuwa na wazo kama hilo kwa sababu hategemei jambo lolote baya kutokea.

Muhimu ni kwamba mtu unapomaliza kutengeneza michoro ya ujenzi kwa mtaalamu kwa maana msanifu wa jengo na mhandisi ni muhimu sana kwamba kuwakutanisha na fundi uliyeamua kumpa kazi hiyo wakaijadili kwa kina ambapo wataalamu hao unaweza kuwapa kazi ya kuchunguza kama fundi huyo ameelewa kwa usahihi kile walichofanya. Ikiwa fundi ameelewa vizuri kilichofanyika unaweza kumwambia kwamba atakuwa chini ya usimamizi wa wataalamu hao ili aongeze umakini lakini ni vyema ukawalipa wataalamu hao wakatembelea maendeleo ya mradi katika hatua kadhaa kuangalia kama kinachofanyika kinaenda kwa usahihi ambapo pia fundi ataongeza umakini akijua kwamba anafuatiliwa muda wote.

Hata hivyo kwa miradi ambayo ni ya ngazi ya kati kwa maana ya kwamba miradi yenye thamani ya kati ya Tshs milioni 100 mpaka Tshs bilioni 1 mtu unaweza kuwapa mkataba wa ujenzi kampuni ya ujenzi ya ngazi ya kawaida yenye wataalamu wote ndani yake. Mradi wako unaweza kufanyika kwa umakini na ubora sana ikiwa utafanywa na kampuni yenye wataalamu wa kutosha wanaofanya kazi kwa viwango sahihi wakizingatia mambo yote muhimu ya kitaaluma. Kama utahitaji msaada wa mapendekezo kwa kampuni nzuri ya ngazi ya kawaida inayofanya vizuri kazi zake kwa ubora na uharaka unaweza kuwasiliana nasi kwa mawasiliano hapo chini.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *