HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUEPUKA UGOMVI NA MWENZA WAKO NA FAMILIA KWA UJUMLA KUHUSU UJENZI WA NYUMBA YENU.

Moja ya kati ya changamoto ambazo nimekuwa nakutana nazo mara kwa mara sana katika kazi za ujenzi na hususan wakati wa kutengeneza ramani za nyumba ni maelewano kati ya wenza juu ya namna wanataka nyumba yao iwe. Japo sio kwa familia zote lakini angalau kwa wengi hutokea hivyo na hasa pale ambapo unakuta mwanaume anaamua lazima mambo yaende anavyotaka yeye halafu mke wake au mwenza wake wa kike anakuwa na vipaumbele vinavyotofautiana na vya mwanaume. Jambo hili limekuwa likileta usumbufu mkubwa kwenye kazi ya kutengeneza ramani ya nyumba yao na wakati mwingine hata kuiharibu au mradi kukwama na kushindwa kuendelea kwa sababu ya malumbano na makubwa na mivutano iliyoshindwa kufikia hitimisho.

Ukweli ni kwamba ni vigumu sana kwa watu wawili hata kama ni mapacha wanaofanana sana mpaka watu wao wa karibu wanashindwa kuwatofautisha ukakuta wanafanana vipaumbele vyao. Binadamu huwa tumetofautiana sana kwa yale tunayopenda au kuyatamani kwa sababu kwanza ya asili, malezi na mambo mengine mengi ambayo yanajumuisha utambulisho wa mtu. Hivyo ni muhimu sana mtu unapoamua kufanya jambo lolote lile ukaanza kwa kuangalia wale linalowahusu na kuona ni kwa njia gani utamaliza utofauti wenu kwa kutumia mbinu za ushawishi kuhakikisha mnajikuta wote kwenye upande mnaoendana.

Kwa hiyo sasa ikiwa mtu unataka kuhakikisha unaepusha mivutano hii na mwenza wako na wengine wanaohusika ni vyema ukazingatia mambo yafuatayo unapouendea mradi wako wa ujenzi.

Kwanza kabisa wazo la kujenga iwe ni la familia au ni la kwako binafsi liwasilishe kwenye familia au kwa mwenza wako kabla ya kuanza kufanya jambo lingine lolote. Kama kuna namna unahitaji sana mapendekezo yako yapite basi yajengee ushawishi kwa kushirikiana na mtaalamu ambaye atasaidia kuyatetea kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu ili kuyaongezea ushawishi kwa mwenza wako na familia kwa ujumla. Mtakaa chini na familia kisha kujadili vipaumbele vyenu hasa kwa kuzingatia utamaduni wenu wa eneo mlilopo kwa wakati husika kisha mtafikia hitimisho wa yale mliyoyaazimia.

Kinachofuata baada ya kuelewana ndipo utatafuta mtaalamu wa usanifu majengo (Architect) ambaye atatoa tena ushauri wa kitaalamu kutokana na mahitaji yenu kwa kulinganisha na taarifa za eneo husika mnalotaka kujenga. Kisha sasa mtaalamu atafanya kazi yake ya kitaalamu kwa kutumia mapendekezo yenu ya kimahitaji kwa kuhusianisha na kanuni za usanifu majengo kadiri ya kila kitu kinavyohitaji kisha baada ya hapo atarudi tena kwenu kufanya uwasilishaji mbele yenu wote.

Family saving money to piggy bank

Baada ya kuwasilisha na mkapata kujua namna mipangilio ya kila kitu ilivyokaa na kufahamu yale yaliyowezekana na yale ambayo bado ni changamoto basi mtafanya tena maboresho na maamuzi kwa kuzingatia ushauri wa mtaalamu ambaye ndiye amefanya uwasilishaji huo. Kitakachofuata baada ya maboresho hayo mtaalamu ataingia kwenye hatua inayofuata ya kutengeneza muonekane wa nje wa jengo maarufu kama 3D kwa ubora na umaridadi mkubwa kisha atafanya tena uwasilishana kwenu ambapo mtatoa maoni, mapendekezo na maboresha ambayo yatafanyiwa kazi ili kufanikisha jengo lenye ubora wa hali ya juu sana.

Kitakachofuata baada ya kukamilisha hatua hizo muhimu mtaalamu atatengeneza michoro ya mwisho ya jengo ambayo itajumuisha kila kitu kinachotakiwa ili kupata vibali vya ujenzi, kusajili mradi kwenye bodi za ujenzi pamoja na kuanza ujenzi wa mradi wenyewe wa ujenzi. Mpaka hapo utakuwa umeepuka kabisa mivutano na ugomvi na mwenza wako pamoja na familia kwa ujumla katika kufanikisha zoezi hili muhimu la kupata makazi yenu bora ya familia na mtu wako. Ikiwa utahitaji ushauri zaidi katika eneo hili na ujenzi kwa ujumla tuwasiliane.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *