HIVI NDIVYO NAMNA HOFU YA KIMAAMUZI INAKULETEA HASARA NA UHARIBIFU KWENYE JENGO LAKO.
- Changamoto ya kufanya maamuzi sahihi kwenye miradi ya ujenzi hasa ya watu binafsi na taasisi binafsi bado ni kubwa sana. Jambo hili linachangiwa na wahusika wenyewe wafanya maamuzi kukosa uelewa wa kutosha juu ya madhara ya maamuzi yao katika miradi yao na hivyo kupelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi ambayo huishia kwenye hasara kubwa na majuto.
- Hofu kubwa inayowakamata watu wengi ni hofu ya kuogopa gharama hivyo kuchagua kufanya kazi na watu wasio na taaluma kubwa wakiamini wanafanya kazi kwa gharama nafuu bila kuangalia madhara yake. Hii hupelekea watu hawa kukwepa wataalamu wenye uwezo sahihi kitaaluma kwa kuona urahisi huo na kuukimbilia wakiamini ndio maamuzi sahihi kulingana na bajeti yake.
- Hata hivyo watu hawa huwa hawana uelewa wakina wa utaalamu wala uelewa sahihi wa gharama wanazokimbia na badala yake huwategemea watu hao hao mafundi kuwashauri bila kujua kwamba watawashauri pale ambapo uwezo wao unaishia na hivyo kujikuta wanafanya makosa ambayo yanaongeza gharama zaidi nah uku gharama za kitaalamu wakiwa hawajui hata ni kiasi gani kulinganisha na hao mafundi wa kawaida waliowaamini na kuwasikiliza.
- Kwa mfano kwa kazi nyingi za kitaalamu ambazo zinafanyika kwa kufuata kanuni za hisabati, sayansi na uhandisi mafundi wa kawaida hutumia ubashiri na uzoefu ambao kutokana na hofu huzidisha sana idadi ili kujihakikishia usalama hata kama itatumia gharama kubwa. Kwa mfano nguzo ambayo kwa mahesabu ya kihandisi ilipaswa kutumia chuma sita pekee za unene wa milimita kumi na sita kuweza kubeba mzigo wa jengo huko juu, fundi kawaida anaweza kushauri ziwekwe chuma kumi za milimita ishirini ili kuhakikisha usalama unakuwepo. Hapo kwa nguzo moja pekee utakuta imechukua gharama mara mbili ya ambavyo ingeweza tu kutosha. Hivyo mfumo mzima wa mhimili ambao ulikuwa ugharimu labda milioni thelathini unakuta unagharimu milioni hamsini. Hapo mtu unakuwa unafikiri umekwepa gharama kwa kukwepa kutumia mtaalamu kumbe ndio umezidisha kwa kusikiliza ushauri kwa mtu ambaye uwezo wake ni mdogo.
- Katika tasnia ya ujenzi pia uongo mwingi na kukosekana kwa uadilifu na utamaduni mbovu huwa kuko zaidi kwa watu wenye uwezo mdogo kuliko watu wenye weledi na taaluma ya juu kwa sababu kwanza wengi wanakuwa wana weledi mkubwa wa kimaamuzi na pia wanajali kuhusu madhara ya maamuzi yao na namna yatawagharimu au kuwawajibisha siku mbeleni. Utamaduni huwa ni tofauti kwa sababu mtaalamu hasa mwenye uzoefu wa miaka angalau kuanzia mitano na kuendelea huanza kuona na kujali zaidi kuhusu kulinda jina na sifa yake ambayo ndio inayompa dhamana ya kuaminika.
- Hivyo ni muhimu sana mtu unapofanya maamuzi ya kuchagua nani na kwa nini ufanye kazi na mtu huyo ni muhimu sana kuzingatia sifa za namna hiyo kwani mara zote majuto huwa ni mwishoni ukiwa umeshaharibu na kupoteza fedha lakini hata ubora au uzuri wa kazi huja mwishoni wakati mradi wenyewe umeshamalizika.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!