KUIBIWA KWENYE UJENZI KUNA MADHARA MAKUBWA, CHAGUA KWA USAHIHI.

Moja kati ya sehemu ambazo huwa na hatari ya kuibiwa ni kwenye miradi ya ujenzi na sababu ni kwa vile wizi wa vifaa vya ujenzi huwa vinalipa sana. Hebu fikiria mtu akifanikiwa kuiba tani moja ya nondo anaweza kupata mpaka kiasi cha shilingi milioni mbili za kitanzania. Kwa kifupi ni kwamba katika ujenzi karibu kila kitu kinaweza kuibiwa na kinalipa sana. Jambo hili limefanya kwamba tabia na utamaduni wa wizi kwa mafundi wa ujenzi kushamiri sana kiasi kwamba limekuwa ni tatizo sugu na ambalo huwapa wamiliki wakati mgumu sana wakati wa ujenzi.

Kwa upande mwingine sasa mtu unaporuhusu kuibiwa huwa unajikuta unaingia hasara kubwa na kupoteza pesa nyingi sana kiasi kwamba sio jambo ambalo unatakiwa kuliruhusu kutokea kwa urahisi kwani litakuacha na madhara makubwa na maumivu makubwa sana pia. Kwa vyovyote vile unapaswa kulinda sana vifaa vya ujenzi katika mradi wako wa ujenzi ili kuhakikisha kwamba uko salama katika hili. Sasa namna ya kujilinda na wizi wa vifaa vya ujenzi katika maeneo ya ujenzi imegawanyika kwa namna tofauti tofauti  

Njia ya kwanza na inayotumia na wengi ni ile ya kununua vifaa na kuvilinda wakati wote wa ujenzi na kuhakikisha kwamba vinavyopaswa kutumika vimetumika na kama kuna vilivyobaki unapanga mwenyewe uvifanyie nini au kuvirudisha dukani. Njia hii ni nzuri lakini inachosha sana kwa sababu utalazimika kupoteza muda mwingi sana kufuatilia na kusimamia kila kitu mwanzo mpaka mwisho. Hata hivyo kwa kuwa wewe sio mtaalamu wa masuala ya ujenzi bado njia hii inaweza isiwe njia sahihi sana kwako kwa sababu mafundi wasio waaminifu bado watashirikiana na wenye maduka kukupotosha na kukuibia au kutafuta upenyo wa namna ya kukuibiwa wakati wa kutumia vifaa hivyo.

Njia ya pili ni njia ya kutafuta watu wenye uaminifu usiotiliwa mashaka na kufanya nao kazi ili kuepuka usumbufu wa kupambana kujiepusha na mbinu chafu mbalimbali za kuchezewa na kupangwa na mafundi ili kuibiwa. Njia hii ni njia nzuri sana kwa sababu licha tu ya kukuepusha kuibiwa lakini pia itakuepusha kudanganywa na kupotoshwa na watu hao. Hata hivyo changamoto ya njia hii kwanza ni kupata watu waaminifu sio jambo rahisi, watu wa aina hiyo kuwapata ni vigumu sana na itabidi utafute sana na kwa umakini mkubwa. Changamoto nyingine ya njia ni kuhadaiwa kwamba watu uliopendekezewa ni waaminifu nawe ukawaamini halafu baadaye unakuja kugundua kumbe haikupewa taarifa sahihi kwani watu hao ni wezi lakini hawajulikani na hakuna mtu yeyote mwenye taarifa kwamba wamewahi kuiba jambo ambalo litakuumiza sana kwani utakuwa umewaamini wezi na kuwaachia ukifikiri ni waaminifu na matokeo yake wanakumaliza kabisa.

Njia ya tatu na pengine sahihi zaidi ni kufanya kazi na kampuni ambayo sio kubwa sana ambayo inafanya kazi za ujenzi kwa gharama nafuu lakini inazingatia utaratibu wote wa kisheria na kusainishana mikataba ya kazi.  Njia hii inaweza kukusaidia kiurahisi endapo utachagua kampuni sahihi ambayo itakupa gharama nzuri na mtaweza kujadili kila kitu na kukubaliana namna mtafanya mradi husika huku mkiwa mmefuata taratibu za kisheria ambapo endapo yeyote atasababisha hasara au ubadhirifu atawajibika kulipa au kufidia hasara yoyote iliyojitokeza. Jambo hili litaongeza umakini sana na tahadhari kubwa kwa kila upande na hivyo kuwa na uhakika wa matokeo yanayotarajiwa.

Karibu sana kwa huduma za ujenzi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *