KUIMARISHA MSINGI WA JENGO(UNDERPINNING)

Hiki ni kitendo cha kuuimarisha kwa kuuongezea ubora na uimara msingi wa jengo lililopo.

Kuimarisha msingi kwa kawaida hufanyika kutokana na mambo yafuatayo.

-Ikiwa jengo linaonyesha dalili ya kuzama chini ardhini au kama linapata nyufa, ambapo ni dalili kwamba msingi uliopo hauna uwezo wa kubeba uzito wa jengo husika.

-Ikiwa jengo linatakiwa kuongezewa ukubwa hasa urefu kwenda juu au kubadilishwa matumizi kwenda shughuli nyingine ambayo itapelekea kuongeza mizigo mikubwa sana ndani ya jengo hilo.

-Ikiwa kuna jengo lingine kubwa lenye msingi mkubwa na mpana au lenye eneo la chini ya ardhi(basement) linatakiwa kujengwa karibu na jengo lililopo ambapo litapelekea matatizo katika jengo lililopo. Hii itasababisha na msingi kutanuka sana na kudhoofisha msingi wa hili jengo lililopo wakati msingi wa jengo jipya unajengwa.

AINA ZA UIMARISHAJI MSINGI(TYPES OF UNDERPINNING)

Kuna Aina Kuu Mbili Za Uimarishaji Msingi

  1. Kuimarisha msingi uliopo
  2. Kuimarisha udongo uliobeba msingi husika

KUIMARISHA MSINGI ULIOPO

-Kuna Aina Nyingi Sana za Kuimarisha Msingi wa Jengo Ila Kwa Hapa Tutajadili Aina Tatu, Kila Moja Hatua Kwa Hatua.

Msingi wa jengo unaweza kuboreshwa kwa namna nyingi na wataalam wa uhandisi wanaweza kubuni njia nyingine zaidi za kuhakikisha uzito wa jengo unabebwa vizuri na ardhi husika.

  1. NJIA YA KUCHIMBA NA KUJAZA.

(i). Hatua ya kwanza ni kujenga msingi wa muda mfupi unaojitegemea kuzunguka msingi uliopo

(ii). Kisha msingi mpya unachimbwa kuzunguka na kwenda chini zaidi ya msingi uliopo ambapo kwa wakati huu msingi uliopo utakuwa haubebi mzigo wa jengo.

(iii). Kisha msingi mpya unajengwa chini ya huu uliopo kwa kujaza zege kwenye msingi uliochimbwa kuzunguka na kwenda chini ya msingi uliopo.

(iv). Baada ya zege la msingi mpya kumiminwa na kukaa sawa ule msingi wa muda mfupi uliowekwa unaondolewa na kuruhusu mzigo wa jengo kubebwa na msingi mpya ulioboreshwa zaidi.

Kitu cha msingi kufahamu ni kwamba hii inafanyika kwa sehemu ndogo ndogo mpaka kukamilika na sio kwa mara moja jengo zima. Kila sehemu inayorekebishwa inaweza kuchukua kati ya mita 2 mpaka 4 kutegemea na ukubwa wa jengo lenyewe. Msingi wa zamani na mpya unaisaidiana kubeba ili kuhakikisha kuna usalama wa kutosha.

Sasa Twende Tuchambue Kila Hatua Kwa Kuingia Ndani Zaidi Ili Kuelewa Kwa Undani.

Hatua Ya Kwanza: Msingi wa muda unajengwa ili kubeba uzito wa jengo, ili msingi uliopo uwe huru kuweza kufanyiwa kazi. Kwa vyovyote hili litaleta changamoto kiasi ndani ya jengo kwa sababu ni lazima sakafu ya chini ya jengo itobolewa katika kuhakikisha uzito wa jengo unalala kwenye msingi mpya. Jengo huanza kushikiliwa na msingi mpya wenye boriti zinazowekwa. Boriti hizi(beams) nyingi zaidi zinawekwa katika umbali fulani wa kutosha kuweza kubeba uzito husika.

Kwa msingi huu wa muda mfupi ni vyema kutumia boriti za chuma zenye muundo wa H ambazo zitaweza kutumika tena katika mradi mwingine. Hizi boriti zikishachomekwa vizuri nafasi kati yake na ukuta wa msingi hugundishwa na saruji nzito ili kuta hizi ziweze kusafirisha uzito kwenda kwenye boriti.

Hatua Ya Pili: Huu msingi wa muda mfupi unapokuwa tayari na kuwa umeshathibitishwa udongo huanza kuondolewa pembeni na chini ya msingi uliopo ambapo msingi uliopo utabaki unaelea hewani. Hili linatakiwa kufanyika kwa makini sana kwani ni jambo la hatari sana. Ni muhimu kujua kwamba njia ya kuimarisha msingi kwa kuchimba inatumika tu ikiwa udongo wa eneo husika ni udongo unaoshikana vizuri ambao hauwezi kuanguka utakupochimbwa ambapo unaweza kuua watu watakaokuwa wanajenga.

Hatua Ya Tatu: Kisha msingi unaimarishwa kwa kujaza zege maeneo yaliyoondolewa udongo. Ni muhimu kuhakikisha kwamba hakuna nafasi inayobaki kati ya msingi wa zamani na mpya ambapo nafasi hizi zikiwepo zitasababisha jengo litalala kwenye hizi nafasi na kusababisha nyufa na ubaribifu katika jengo. Hivyo kujaza zege kila mahali bila kuacha nafasi kabisa ni muhimu sana.

Hatua Ya Nne: Zege likishamiminwa vizuri na kutulia, huu msingi wa muda uliowekwa unaweza kuondolewa maeneo yaliyochimbwa ili kuuweka kisha yanafukiwa na sakafu iliyoharibiwa inatengenezwa upya na kukarabatiwa. Zege hili lililowekwa ni kubwa, limeimarisha sana msingi na kulala kwenye udongo kwa kina kirefu zaidi na kupelekea usalama mkubwa zaidi kwa jengo.

Kazi nzima inafanywa kwa vipande vipande. Kwa mfano kama jengo lina urefu wa mita 30, basi kazi hii inaweza kufanywa kwa vipande vya mita tatu tatu mpaka kukamilisha.

  • NJIA YA BORITI LILILOTENGENEZWA (NEEDLE BEAM METHOD)

Hii inafanywa kwa hatua zifuatazo

(i). Tengeneza nguzo mbili imara zinazokwenda chini sana(micropiles) zilizoko umbali fulani kutoka kwenye jengo. Hizi hujengwa kwa kutumia mashine maalum ya kuzijenga(micropile rig).

(ii) Kisha toboa shimo lenye ukubwa wa kutosha kupokea boriti hiyo(need beam)

(iii) Tengeneza hiyo boriti(needle beam) juu ya nguzo hizo inayopita katikati ya kuta za msingi wa jengo ndani ya msingi

(iv) Baada ya kukamilisha kujenga hiyo boriti(needle beam) jaza udongo juu ya boriti hilo(needle beam). Baada ya hapo msingi utakuwa imara vya kutosha kubeba uzito uliokusudiwa.

Njia hii ina faida ya kutoleta usumbufu ndani ya jengo.

Tujadili hatua zake:

(i). Tumia mashine ndogo maalum ya kutengeneza nguzo imara zinazokwenda chini sana(michopiles) kutengeneza nguzo hizi karibu na jengo. Kwanza angalia kwa makini kwamba jengo lisiwe dhaifu sana ili mitetemo inayotoka kwenye mashine ya kutengeneza nguzo hizi isisababisha maafa kwenye jengo.

(ii). Toboa eneo ambalo boriti itajengwa kisha toboa shimo lenye ukubwa wa kutosha kupokea boriti hii inayotokeza kwa nje pande zote inayopita katikati ya kuta za msingi ndani ya msingi wa jengo.

(iii). Mwaga zege yenye nondo inayotokeza pande zote mbili za jengo(RCC cantilever needle beam), hakikisha kuna muunganiko sahihi kati ya nguzo hizi(micropile) na boriti(beam).

(iv). Jaza udongo maeneo yaliyowazi, unakuwa umemaliza.

  • NJIA YA KUTUMIA NGUZO IMARA ZILIZOKWENDA CHINI SANA: MICROPILING METHOD

(i). Tengeneza nguzo imara inayokwenda chini(micropile) sana iliyopo chini ya msingi wa nyumba uliopo

(ii). Chimba na ondoa udongo mpaka utakapoikuta nguzo hiyo uliyoweka iliyopo chini ya msingi

(iii). Kisha ondoa udongo uliopo kati ya nguzo hiyo na msingi wa jengo ambapo iatatengeneza ombwe/nafasi iliyopo kati ya nguzo na msingi.

(iv). Jaza ombwe/nafasi hii kwa zege. Ikishakaa sawa tayari msingi uliopo unaweza kupeleka mzigo wa jengo kwenye nguzo hizo na kuongeza sana uwezo wa jengo kubeba uzito mkubwa.

TUCHAMBUA KWA KINA HATUA KWA HATUA.

Hatua 1; Tumia mashine maalum(micropile rig) ya kutengeneza nguzo hizi imara zinazokwenda chini sana chini ya msingi uliopo. Kabla ya kufanya hivyo mtu anatakiwa kuchimba kwenda chini eneo lililopo katibu na msingi ili kujenga kwa uhakika msingi umeenda chini kiasi gani.

Hatua 2; Chimba sehemu ya udongo mpaka kufika juu ya nguzo hii iliyojengewa chini ya msingi kuhakikisha kuna eneo la kutosha kufanyia kazi.

Hatua 3; Ondoa udongo kati ya nguzo hii iliyojengwa kwenda chini(micropile) na msingi wa jengo uliopo.

Hatua 4; Jaza nafasi hii kwa zege. Endelea kurudia kufanya hivyo kila baada ya umbali fulani mpaka kukamilisha msingi wote.

Na Architect Sebastian Moshi

Mawasiliano +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *