MALIGHAFI ZA UJENZI – ZEGE
Tunapozungumzia zege kwenye swala zima la ujenzi huwa tunamaanisha zege lenye chuma ndani yake(reinforced concrete). Kitaalamu inajulikana kama “reinforced cement concrete”, au RCC. RCC ni zege ambayo ndani yake ina nondo au chuma zinazojulikana kama nondo za zege. Huu mchanganyiko wa chuma na zege hufanya kazi vizuri sana na huwa imara sana kwa sababu haivunjiki au kukunjika kiurahisi.
Kutengeneza zege hili kwanza hutakiwa kutengeneza umbo linalounda sehemu ya zege inayotengenezwa kwa kutumia mbao au bati kisha kukunja chuma na kuzifunga kwa nondo nyembamba na kuzitumbukuza katika umbo la mbao au bati ulilotengeneza linalojulikana kama “formwork”. Baada ya kutengeneza “formwork” unachanganya kokoto, mchanga, saruji na maji kwa kiwango kilichopendekezwa kadiri ya uimara unaohitajika kisha kumimina katika hizo “formworks” zenye nondo ndani na baada ya masaa kadhaa inakuwa imeshakuwa ngumu. Hata hivyo ili kuweza kupata uimara wa kutosha kudumu kwa miaka mingi itapaswa kumwagiliwa maji mara kwa mara kila siku kwa siku zisizopungua 21.
AINA ZA ZEGE
Zege Lenye Uimara wa Juu – Hii ni aina ya zege ambayo ni imara kiasi kwamba haiwezi kubonyezwa na mzigo wowote ikabonyea kiurahisi hivyo inaweza kumudu mzigo mkubwa bila kupungua upana wake.
Zege Lenye Ubora wa Hali ya Juu – Hii ni aina ya zege ambayo imetengenezwa miaka ya hivi karibuni ambayo inafanya vizuri katika nyanja nyingi na kuizidi aina za kawaida za zege zilizotengenezwa kama vile kudumu muda mrefu, kutoathiriwa na kemikali za kimazingira zinazoathiri zege, uwezo wa kuruhusu maji, uzito n.k.
Zege Jepesi – Hii ni aina ya zege ambalo huwa jepesi na hutengenezwa kwa na kokoto ndogo ndogo sana na nyepesi. Aina hii ya zege hutumika kwenye maeneo ambayo sio sehemu za mfumo wa mihimili ya jingo husika, ambapo mara nyingi hutumika kama ukuta au kuta za kugawa nyumba na mara nyingi zaidi hutumika kutengeneza urembo au maumbo yanayotengeneza muonekano sahihi wa jengo kama ilivyoamuliwa na msanifu wa jengo.
Zege Lisilopitisha Maji – Hii ni aina ya zege ambalo hutengenezwa kwa punje ndogo ndogo sana za mchanga na saruji ambalo haliruhusu kabisa maji kupita. Hili huwa zege maalumu kwa ajili ya kujengea vitu ambavyo havitakiwi kuruhusu maji kupita kama vile mabwawa ya maji, matenki ya maji, kuta zinazojengwa kwenye kingo za maji, kuta zinazojengwa ndani ya maji kama vile chini ya bahari, mto au ziwa n.k.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!