NUNUA MABATI KIWANDANI KUPUNGUZA KAZI NA KUEPUKA KUPOTEZA.

Katika kazi za ujenzi kuna mambo mengi ambayo huwa hayafikiriwi kwa usahihi hata kama mazingira yanaruhusu kwa sababu aidha ya kutokujua, kutokujali au kutoweka umakini kwenye kazi. Moja kati ya mambo ambayo hukosa umakini ni suala la kununua mabati. Mabati kwa sehemu kubwa yanauzwa kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi na ndipo watu wengi hununua kwa sababu mbalimbali. Lakini mabati haya huuzwa kwa moja moja zima, na hilo ni sahihi kabisa ikiwa hilo ndilo unalotaka. Lakini unapokuja kuyaezeka kwenye nyumba mabati sio yote utayaezeka yakiwa mazima, kuna mengi ambayo utayakata vipande vya aina tofauti tofauti ili yaenee sehemu husika kadiri ya muundo wa paa lenyewe ulivyokaa.

MABATI HUKATWA KIWANDANI KADIRI YA UHITAJI

Sasa, hivi vipande unavyokata kwa sehemu kubwa ni upotevu wa rasilimali na hasara kwa sababu utaendelea kununua mabati zaidi ili yaenee huku mengine ukiyakatakata na kutupa. Kwa hiyo ili kuepuka huu upotevu na hasara unaosababishwa na kutumia njia hii ya mazoea, ikiwa unajua kiwanda kinakopatikana na urahisi wa kukifikia, unapaswa kukaa chini na fundi wa paa au mhandisi mkaandika idadi na saizi za mabati zinazohitajika kwa paa husika kisha ukaenda kiwandani na kutengenezewa yale unayohitaji kwa saizi unayohitaji peke yake bila kulazimika kuchukua mazima yatakayohitaji kuyakata na kutupa vipande.

UTAPUNGUZA GHARAMA

Kwa maana hiyo utakuwa umeepuka kununua zima kwa gharama kubwa kisha kukata na kutupa sehemu, pamoja na kupunguza kazi hiyo ya kukata, lakini pia bei ya kiwandani itakuwa nafuu zaidi kuliko ya dukani ikiwa gharama za usafiri zinalingana na usumbufu wa kiwandani sio mkubwa.

Architect Sebastian Moshi.

WhatsApp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *