UJENZI WA GHARAMA NAFUU WA KUWA NAO MAKINI

Kuna kundi kubwa la watu ambao wanaogopa sana gharama za ujenzi na wanafikiria sana namna ya kufanikisha ujenzi kwa gharama ndogo ya njia ya mkato ambayo wanaamini ipo na wanaweza kufanikisha kujenga kwa urahisi sana. Watu wa kundi hili kwa kuwa wanatamani sana kupata njia ya mkato ya kufanikiwa kujenga kwa gharama nafuu sana wanakuwa rahisi kumsikiliza na kumwamini yeyote anayewaambia kwamba anaweza kuwafanikisha ujenzi kwa gharama nafuu sana kwa sababu ndicho wanachotafuta kukisikia na kukiamini.

BAADHI YA WATU WAKO TAYARI KUSEMA UONGO ILI WAFANIKISHA KUPATA FEDHA KIDOGO NA KUACHANA NA MRADI WENYEWE

Sasa wapo watu wengi na hasa mafundi katika fani hii ya ujenzi ambao sio waaminifu na wenye kupenda kutumia fursa hii ya uwepo wa watu wa kundi hili kufanikisha malengo yao ya muda mfupi huku wakimwacha mteja husika kwenye mataa. Watu hawa humwaminisha mteja kwamba mradi wake unaweza kufanyika kwa bei rahisi sana na hata wao wenyewe wako tayari kulipwa kidogo kufanikisha kazi hiyo vizuri kabisa. Lakini watu hawa moyoni mwao hujua wazi kabisa kwamba wanachoongea ni uongo na jengo hilo haliwezi kujengwa kwa gharama wanayosema tena pengine hata mara mbili ya gharama haitoshi, lakini wao hawajali kwani lengo lao ni wapewe kazi hiyo, ambapo watalipwa pesa ya kuanzia kazi na kisha wataianza kazi husika na kuifanya kidogo kisha kuachana nayo huku wakimwacha mteja akiwa hajui cha kufanya.

FUNDI HUTOA SABABU YA MSINGI KABISA YA KUAMUA KUACHANA NA MRADI WAKIJUA KWAMBA HAWATAWEZA KUUKAMILISHA KWA GHARAMA WALIYOTAJA

Mteja aliamini kwamba milioni 20 itamaliza kazi yake na atahamia lakini pengine baada ya kumaliza msingi tu fundi husika anaikimbia kazi na kusema hataki tena kuendelea nayo kwa sababu zozote zile, kumbe lengo lake lilikuwa kupata pesa kidogo alizopata ili zimtatulie changamoto zake za muda huo kisha hakai muda mrefu kwenye kazi hiyo kabla hajaachana nayo. Hivyo ni vyema kuwa makini sana na wajenzi au mafundi wanaokubali kushusha sana gharama zao ili ukubali kuwapa kazi kwani unaweza kujikuta unajilaumu siku za usoni.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *