GHARAMA ZA MICHORO YA RAMANI NI SEHEMU YA GHARAMA ZA UJENZI.

Watu wengi wamekuwa wakilalamikia sana gharama za michoro ya ramani katika ujenzi kwa sababu kwanza wamekuwa wakiamini ni gharama kubwa sana na hazistahili. Moja kati ya sababu zinazopelekea wao kuamini kwamba gharama za michoro ya ramani za ujenzi ni kubwa ni kwa kuwa wanafikiri kazi ya kutengeneza ramani ya ujenzi ni kazi rahisi na ya muda mfupi isiyotumia muda wala akili sana katika kuifanya ambapo wengine wamekuwa wakifikiri ni kazi ya kumaliza ndani ya lisaa limoja, kwa kifupi wamekuwa na mtazamo fulani juu ya kazi nzima ya kutengeneza michoro ya ramani za ujenzi.

MICHORO YA RAMANI INAHUSISHA SETI 7 ZA MICHORO AMBAZO ZITAKUWA PRINTED KATIKA NAKALA NGUMU TATU

Jambo la kwanza kufahamu ni kwamba ramani ya ujenzi ni sehemu ya mradi wa ujenzi, kwa hivyo kama kujenga nyumba ya kuishi ya vyumba vitatu itagharimu Tshs milioni 80 basi gharama za kutengeneza ramnai za ujenzi ni sehemu ya hiyo Tshs milioni 80, tena ikiwa ni sehemu muhimu sana inayotoa miongozo yote ya kazi nzima itakavyofanyika na kila anayeenda kuhusika kwenye kazi hii hata kama ni mwanataaluma mwingine au fundi atategemea michoro ya ramani kwanza ili kufanikisha kazi yake. Hivyo kama vile unavyoweza kufikiria namna utamlipa fundi anayepiga jengo ripu au fundi anayepaua unatakiwa kumfikiria anayetengeneza michoro ya ramani kwani yeye ndiye anayetoa mwongozo hata kwa hao wanaofanya hayo mengine yote yanayofuata. Lakini pia kazi ya kutengeneza michoro ya ramani sio kazi rahisi wala sio kazi ya siku moja, kwa nyumba ya kawaida ya kuishi isiyo ya ghorofa kwa wastani mtu akijitahidi anaweza kutumia wiki nzima kukamilisha kazi yote ambayo kwa kawaida inajumuisha seti saba za michoro mbalimbali. Lakini kazi hii inahusisha ubunifu na kufikiria sana, pia inatumia programu mbalimbali za kompyuta kutengeneza picha za mionekano mbalimbali na mwisho kuandaa michoro yenyewe baada ya kukamilisha “concept” yenyewe. Ni hatua tatu kubwa ambazo zote zinachukua muda mrefu ambao sio pungufu ya siku mbili kila hatua kwa kufanya mfululizo ikiwa mtu anataka kufanya kazi iliyo katika viwango bora.

JENGO LINALOFANYIKA KATIKA VIWANGO SAHIHI HALIWEZI KUFANYIKA KWA MASAA, LAZIMA LITAHUSISHA UTAFITI NA TAFAKARI ZINAZOCHUKUA MUDA.

Mwisho kabisa kwa kutumia kanuni ya asili thamani ya jengo inapaswa kuwa na uwiano sahihi wa thamani ya huduma zizokwenda kulifanikisha jengo husika, kwa mfano kama vile kupiga jengo plasta inaweza kugharimu 3% ya gharama zote za ujenzi basi gharama za kutengeneza michoro ya ramani ya jengo zinatakiwa kuwa katika uwiano huo huo ili kulijenga jengo katika hadhi inayostahili, tofauti na hivyo lazima utakuwa unatafuta matatizo mengine yanayoweza kuja kukugharimu zaidi baadaye.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *