FAHAMU GHARAMA ZA UJENZI KWA UZOEFU WA MIRADI MINGINE.

Kufahamu gharama halisi za ujenzi wa mradi wa jengo au nyumba ya ukubwa wowote ule imekuwa ni changamoto sio tu kwa wateja bali hata kwa wataalamu ndani ya fani ya ujenzi yenyewe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kubadilika kwa gharama za vifaa vya ujenzi na hata kushuka kwa thamani ya fedha. Lakini pamoja na kwamba suala la kufahamu gharama halisi za ujenzi bila kutumia wataalamu ambao nao wanatumia miongozo mbalimbali inayotolewa na taasisi mbalimbali za umma na binafsi limekuwa ni changamoto kwa wengi bado watu wengi huwa wana mahesabu yao wenyewe kichwani na hivyo wanapopewa makadirio ya gharama za ujenzi huo imekuwa vigumu kuamini au kukubaliana na gharama husika. Hata hivyo licha ya kwamba gharama za ujenzi hutegemea na aina ya vifaa na huduma unayochagua lakini bado watu wengi wamekuwa wagumu kuamini hata gharama za huduma za viwango vya wastani.

WASTANI WA GHARAMA ZA UJENZI UNAWEZA KUUFAHAMU KWA KUPITIA MRADI WA UJENZI ULIOKAMILIKA

Sasa ili kuweza kupata picha ya wastani wa gharama za ujenzi wa jengo/nyumba yako unaweza kutafuta mradi ambao umeshakamilika na umefanyika siku za hivi karibuni kisha kuonana na mhusika mwenye jengo na kumwomba akusaidie kufahamu gharama za nyumba hiyo kwa kuorodhesha idadi ya vifaa vyote vilivyotumika kisha kutafuta bei zake madukani kwa kuwasiliana na watu wa maduka ya vifaa vya ujenzi na maeneo mengine wanakouza vifaa vya ujenzi pia. Kisha utaomba kujua gharama za ufundi zilizotumika kwenye kila hatua ya ujenzi kisha utajumuisha mahesabu yote na kupata wastani wa gharama ambayo nyumba yako inaweza kwenda kugharimu. Katika kuchagua nyumba unayokwenda kuifanya kama mfano wa kuweza kujua gharama hakikisha inakaribia ukubwa na aina ya nyumba kuendana ambayo unataka kwenda kuanza kujenga. Hili litakusaidia wewe mwenyewe kukaa kwenye uhalisia na kuepuka kujidanganya na kudanganywa, na utajua kwa hakika haswa kile unachokwenda kufanya kwa upande wa idadi ya vifaa na gharama.

KUSHINDWA KUFAHAMU GHARAMA HALISI ZA UJENZI KUNAWEZA KUPELEKEA MRADI KUISHIA KATIKATI NA KUWA HASARA KUBWA

Taarifa zisizo sahihi juu ya gharama za ujenzi ambazo watu wengi hupendelea kuziamini kwa sababu zinawafurahisha huishia kuwaumiza au kuwapoteza na wakati mwingine wanashindwa kabisa kumaliza mradi husika wa ujenzi kwa sababu ya kutochukua jukumu la kufahamu uhalisia kiundani.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *