KINACHOLIPIWA KWENYE HUDUMA ZA USHAURI WA KITAALAMU NA UJENZI NI MUDA NA THAMANI.
Kati ya vitu ambavyo vimekuwa vikishangaza sana duniani katika Ulimwengu wa biashara ya soko huria ni jinsi vitu vinaweza kutofautiana bei licha ya kufanana kabisa matumizi. Lakini licha ya baadhi ya watu kufikiri kuna tatizo lakini wale ambao wanaelewa namna asili inavyofanya kazi yake hawashangazwi na hilo kwa sababu asili siku zote huwa ina nguvu sana na kuishinda sio kazi rahisi.
Habari njema ni kwamba mara nyingi utofauti huu wa bei hauwezi kuwepo bila sababu na kama kutakuwa hakuna sababu basi huduma husika haiwezi kudumu katika mafanikio. Sababu kuu mbili zinazopelekea utofauti huu ni utofauti wa thamani baina ya bidhaa au huduma husika na sababu ya pili ni uhaba wa wa bidhaa au huduma hiyo japo kwa dunia ya leo uhaba wa vitu umekuwa hadimu zaidi.
Watu wamekuwa wakishangaa kwa nini huduma ile inakuwa na gharama zaidi ya huduma nyingine ya kitu kile kile na sababu ni kwanza muda wa mtu husika ambao anauweka kwenye kazi hiyo baada ya kuachana na mambo mengine yote ni lazima anaangalia thamani ya muda wake kama unaendana na gharama anayolipwa au autumie kwenye kazi nyingine yenye kumlipa zaidi na pili ni kiwango cha thamani anachokitoa kama kinaendana na kiasi cha gharama hiyo.
Uhalisia huu upo zaidi kwa asili na mara nyingi thamani inayotolewa kwa sehemu kubwa huwa haitofautiani sana na kiasi cha gharama kinacholipwa. Hili linaweza kuonekana hata kwenye kazi kwamba kuna mtu analipwa mshahara hata mara 10 zaidi ya mtu mwingine katika ofisi moja na wote wakiwa na elimu na umri unaolingana katika kazi. Hiyo ni nguvu ya asili ambayo kwa haraka haraka watu huwa hawaioni na kufikiri pengine kuna kitu hakipo sawa au kuna upendeleo fulani.
Kwenye ujenzi napo mambo hayako tofauti sana, thamani ya huduma hizi kuanzia huduma za ushauri wa kitaalamu mpaka huduma za ujenzi wenyewe huendana na thamani ambayo hutolewa, kuanzia kwenye suala la usimamizi, muda na ubora wa kiufundi katika kazi husika na thamani yake huweza kuonekana katika maeneo yote hayo.
Hivyo mtu anapofikiria kulipia huduma hizi ni muhimu kuhakikisha ubora wake na kulinganisha beo kutokana na ubora wake badala ya kufananisha na kufikiri labda kuna kitu hakikaa sawa kwa sababu hili lipo kwenye kila bidhaa au huduma unayolipia kwa mfano simu janja zinatofautiana bei zipo kuanzia za Tshs 100,000 mpaka za Tshs 5,000,000 hali kadhalika magari ni hivyo hivyo, nguo n.k. Jambo la msingi ni kujiridhisha kwamba kweli huduma husika ina thamani ya gharama unayolipia usije ukawa umeibiwa.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!