GHARAMA ZA KUWEKA BANGO LA UJENZI NI KUBWA KULIKO GHARAMA ZA KIBALI.

Kwa siku hizi suala la mtu kuwa na kibali cha ujenzi kwanza kabla ya kujenga limeendelea kuwa ni la muhimu na la lazima kwa maeneo mengi Tanzania hususan yaliyopo ndani ya halmashauri za miji, manispaa na majiji. Lakini mbali na kupata kibali cha ujenzi pia kuna utaratibu wa kuweka kibao cha ujenzi ambacho kinaonyesha wataalamu wanaohusika kwenye mradi husika hususan kwa majengo ya ghorofa.

Katika vibali hivi viwili ambacho huwa ni muhimu sana na cha lazima zaidi ni kibali cha ujenzi kinachotoka halmashauri kwa sababu hicho kinapatikana baada ya michoro na mradi tarajiwa kukaguliwa na idara zote za halmashauri kuhakikisha kwamba mradi husika umekidhi vigezo vyote muhimu vya idara zote husika zilizopo katika halmashauri husika.

Kibali cha ujenzi kutoka halmashauri huchukua muda kidogo kupatikana, huwa na masharti mengi na usumbufu kiasi kadiri ya mradi unavyokuwa umekidhi vigezo vinavyotakiwa lakini gharama yake ni ya wastani ukilinganisha na gharama za kufanikisha kuweka bango la ujenzi katika eneo la mradi linaloonyesha wataalamu wote wanaohusika katika mradi husika.

Gharama ya kuweka bango la ujenzi katika eneo la mradi zinategemea na wingi wa wataalamu ambao mtu anawatumia katika mradi husika. Hii kwa sababu kwa kila mtaalamu mmoja atakayehusika katika mradi husika itatakiwa kununuliwa stika inayowakilisha taaluma yake kutoka kwenye bodi ya taaluma husika, pamoja na kampuni ya mtaalamu huyo kulipwa kiasi cha pesa ambacho mmepatana kama fedha za ushauri wa kitaalamu kwenye hatua ya usimamizi ili aruhusu jina la kampuni yake kutumika ikiwa hujamwajiri moja kwa moja kama msimamizi mkuu.

Hivyo kila mtaalamu mmoja atatakiwa kulipwa fedha za ushauri wa kitaalamu katika usimamizi wa mradi husika baada ya stika kutoka kwenye bodi ya taaluma husika kuwa imenunuliwa. Kwa kawaida huwa kuna taaluma nyingi kama vile usanifu majengo, uhandisi mihimili, ukadiriaji majenzi, ukandarasi, uhandisi umeme, uhandisi huduma n.k., ambapo zote hizi huweza kuhitajika.

Hata hivyo kwa majengo yaliyo mengi ambapo mengi sio majengo makubwa sana taaluma tatu kati ya hizi ndio huwa muhimu ambazo ni usanifu majengo, uhandisi mihimili na ukadiriaji majenzi na ikiwa jengo ni kubwa kidogo na ukandarasi pia huweza kuongezeka.

Kwa maana hiyo hapa itabidi kudili na wahusika wa taaluma hizi ili kuweza kufanikisha kununua huduma zao kwa makubaliano fulani maalumu na hivyo kufanikiwa kukamilisha uwekaji wa bango la ujenzi katika eneo la mradi huku ukipata sehemu ya huduma zao za usimamizi. Hivyo kwa vyovyote vile gharama hizi huwa kubwa hata mara kumi zaidi ya gharama za kupata kibali cha ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *