KUNA MAKOSA KWENYE UJENZI AMBAYO HAYAWEZA KUONDOLEWA NA UKARABATI.

Kama tunavyoendelea kusisitiza siku zote kabla ya kuanza ujenzi wa nyumba yako au jengo lako jambo la kwanza kabisa na muhimu sana kufanya ni kukutana na mtaalamu wa ujenzi kwa upande wa usanifu majengo na uhandisi ili kujadili mradi wako ambao utakufaa wewe kwa maana ya kukuvutia na kuendana na mahitaji yako. Hii ndio hatua ya kwanza kabisa na muhimu sana pale unapofikiria kujenga.

Baada ya kupata ushauri na kufanya maamuzi sahihi kadiri ya vipaumbele vyako na kuweza kukamilisha zoezi la kutengeneza michoro ya ramani inayokidhi mahitaji yako pamoja na mahitaji ya kitaaluma kitu muhimu kitakachokuwa kinafuata ni hatua ya kuanza ujenzi. Hapa napo hupaswi kufanya makosa utakayokuja kuyajutia, unapaswa kuhakikisha kwamba kunakuwa na usimamizi makini wa mradi wako utakaozingatia viwango sahihi vya ubora.

Hatua hizi kubwa mbili muhimu ni za kuzingatia sana kwa sababu kuna makosa yakishafanyika hayawezi kuondolewa na ukarabati na hata kama kwa kiasi fulani yanaweza kupunguzwa athari zake kupitia ukarabati bado yatakuja na gharama kubwa sana. Hivyo japo matokeo yanaweza yasionekane kwa haraka lakini kutoa kipaumbele kwa viwango vya ubora kutapelekea kazi yako kukuepusha na hasara na majuto ya muda mrefu pale ambapo kuna mambo utashindwa kuyarekebisha hata kwa gharama kubwa pale utakapohitaji.

Makosa kama muonekano usiovutia uliosababishwa na mpangilio usio sahihi wa vipengele vya jengo huwa ni aidha vigumu sana kubadilisha au kushindikana kabisa kupata kile hasa unachotamani kukipata. Au mpangilio usio sahihi wa jengo katika kiwanja ambapo limejengwa ni makosa ambayo hayawezi kurekebishika na hivyo utalazimika kuishi na mapungufu hayo katika kipindi chote cha maisha ya jengo husika kitu ambacho kinaweza kukupa majuto ya wakati wote.

Hivyo katika kuepuka changamoto hizi usikubali kabisa kufanya kazi kienyeji bila kuzingatia kanuni muhimu sahihi za kitaalamu na kuhusisha watu wenye uwezo ili kuepuka kufikia hatua ambayo utashindwa kufanya marekebisha na kuishia kwenye majuto.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *