JENGO LAKO LITAENDELEA KUANGUKA TARATIBU.
Wiki iliyopita tumeshuhudia jengo la ghorofa likiporomoka maeneo ya Goba jijini Dar es Salaam na kusababisha majanga ya vifo vya watu wanne pamoja na majeruhi 17. Ni wazi kwamba kuanguka kwa jengo hilo ni matokeo ya kukosekana kwa utaalamu makini uliozingatiwa katika hatua zote muhimu katika ujenzi kuanzia katika hatua ya utengenezaji wa michoro ya ramani mpaka katika hatua ya usimamizi unaozingatia taratibu zote muhimu.
Licha ya kwamba kuanguka kwa jengo wakati ujenzi unaendelea ni matokeo ya uzembe uliopitiliza lakini watu wasichojua ni kwamba uzembe haupo tu pale ambapo jengo linaanguka haraka peke yake, bali kuna uzembe mwingine mwingi unaoendelea lakini ambao madhara yake hayaonekani kwa haraka. Jengo lako linawez lisianguke leo kwa sababu makosa sio makubwa sana lakini udhaifu uliopo unalifanya liendelee kuanguka taratibu.
Kazi za ujenzi ambazo hazifuata viwango sahihi vya kitaalamu kuanzia hatua ya mwanzoni kabisa wakati wa kutengeneza michoro ya ramani mpaka katika hatua ya ujenzi wakati wa kujenga huwa na udhaifu ambao matokeo yake yataendelea kuja taratibu na kwa sehemu kubwa yatakuwa yanadhibitiwa kupitia ukarabati wa mara kwa mara ambao unahusisha gharama kubwa pia lakini bila kumaliza tatizo kwa sababu makosa makubwa yalishafanyika mwanzoni.
Hivyo kabla ya kushangaa na kuona kwamba kuna uzembe mkubwa umefanyika katika kazi jengo lile la ghorofa la huko Goba ni muhimu kujiuliza endapo nawe ujenzi wako umezingatia utaalamu ambao umehakikisha uimara unaoweza kuliokoa jengo sio tu wakati wa kujenga au miaka michache baadaye bali kwa miaka mingi sana baada ya jengo kukamilika. Kama jengo lako matokeo ya udhaifu wake yataanza kuonekana baada ya miaka 10 hakuna sababu ya kucheka jengo lililoanguka kwani uzembe ule unatofautiana kidogo na uzembe wako pia.
Ni muhimu sana kuzingatia ushauri wa kitaalamu na kutumia wataalamu katika mradi wako wa ujenzi ili kuepuka hasara, majuto na hata majanga makubwa ya vifo na ulemavu kama hayo yaliyotokea. Hii ni kwa sababu matokeo ya ubovu au udhaifu wa jengo kwa sehemu kubwa hayaonekani kwa haraka bali yatakuja kutokea baada ya miaka kadhaa hivyo sio rahisi kuona wakati unajenga ambapo utajikuta unajifariji kwamba uko salama kumbe majanga na majuto yako mbeleni.’
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!