KINACHOSABABISHA CHANGAMOTO YA NYUFA KWENYE NYUMBA.
Nyufa katika kuta za majengo huweza kutokea kwa sababu mbalimbali zikiwemo udhaifu wa malighafi za ujenzi zilizotumika, ujenzi wa viwango duni, njia zisizo sahihi za ujenzi, mabadiliko ya hali ya hewa n.k., Hata hivyo licha ya kwamba kuna nyufa ambazo ni hatari kwa uimara wa jengo na uhai wa watumiaji lakini sio nyufa zote ni hatari. Kuna nyufa nyingi ambazo hazina hatari yoyote na hupaswa kufanyiwa ukarabati kuzifunika ili kuboresha muonekano wa jengo lakini hazina hatari yoyote. Hata hivyo huwa kutambua nyufa hatari na sisizo hatari wakati mwingine sio kazi inayoweza kufanywa na mtu yeyote badala yake anatakiwa kupatikana mtaalamu mbobezi wa kutafiti ufa wenyewe kujua kama ni hatari au ni ufa wa kawaida.
SABABU KUU ZA NYUFA KWENYE MAJENGO.
1. Kudhoofika/kunyong’onyea kwa vifaa/malighafi zilizotumika kwenye ujenzi.
Kwa mfano ikiwa kama tofali zilijengwa kwa kiwango cha chini sana au ile saruji inayounganisha tofali ilitengenezwa kwa uwiano hafifu sana wa malighafi zake basi uzito wa jengo kutokea juu unaweza kukandamiza sana na kupelekea nyufa kwenye jengo. Lakini hata hivyo wakati mwingine bila hata mkandamizo unaotokana na uzito wa jengo kutokea juu bado nyufa zinaweza kutokea kwa vifaa/malighafi zenyewe kunyong’onyea kutokana na udhaifu wake wenyewe wa ndani.
2. Kutanuka na kusinyaa kwa vifaa/malighafi za ujenzi kutokana na mabadiliko ya joto.
Vifaa/malighafi zote zinazotumika kwenye ujenzi hutanuka kutokana ongezeko la joto na kusinyaa kutokana na ongezeko la hali ya baridi ambavyo hutokea ndani ya siku moja. Kwa kawaida nyakati za mchana joto huwa kali na nyakati za usiku hali ya baridi huongezeka sana, hali hii ya kutanuka na kusinyaa kwa haraka kwa malighafi za ujenzi huchangia kwa sehemu kubwa sana kusababisha nyufa kwenye majengo. Hata hivyo nyufa zinazotokana na kutanuka na kusinyaa kwa malighafi za ujenzi zinategemea na aina na viwango vya kemikali zilizotumika kutengeneza malighafi hizo.
3. Mgandamizo unaotokana na uzito wa mizigo hai au mfu katika jengo.
Kwa kawaida mizigo ya kwenye jengo hupimwa ili kuweza kumudu migandamizo na mizigo ambayo inalazimika kubebwa, lakini pia licha ya kuweza kumudu inapaswa na sifa ya kuweza kurudi katika hali ya kawaida ikiwa mizigo hiyo imepunguzwa au kuondolewa(elasticity). Malighafi iliyotumika kujengea inapokosa sifa ya kuweza kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya mgandamizo(elasticity) ndio hupelekea nyufa katika jengo. Hivyo jengo kwa ujumla katika kutengeneza michoro ya mihimili ya jengo husika ni muhimu sana kuzingatia sifa ya kuhakikisha malighafi zote na vipengele vyote hususan vile vinavyotengeneza mihimili ya jengo vinakuwa na sifa ya kutanuka na kurudi katika hali yake(elasticity). Itaepusha kuvunjika na kusababisha nyufa.
4. Mabadiliko ya kikemikali katika vifaa/malighafi za ujenzi(Chemical reactions).
Kuna aina nyingi za mabadiliko ya kikemikali(chemical reactions) katika majengo ambayo huathiri sana uimara wa jengo. Mabadiliko haya ya kikemikali husababisha kuongezeka kwa ukubwa wa malighafi husika na kusababisha mgandamizo wa ndani ambao hupelekea kusababisha nyufa katika jengo. Lakini pia mabadiliko hayo (chemical reactions) ndani ya malighafi hizo hudhoofisha sana malighafi hizo na kupelekea kunyong’onyea na kusababisha nyufa katika jengo. Sababu zinazopelekea mabadiliko hayo ya kikemikali katika jengo ni kuchanganyika au kuingia kwa kemikali mbalimbali ambazo husababisha mwitikio(reactions) zinapokutana na kemikali nyingine katika jengo. Kwa mfano chuma kutokeza nje ikapata unyevu na kukutakana na hewa moja kwa moja inasababisha kutu ambayo hupelekea kuanza kuoza kwa chuma hiyo na kudhoofisha ule mhimili husika ulioshikilia jengo.
5. Aina ya udongo uliotumika kurudishia wakati wa kujenga msingi wa jengo.
Kuna aina za udongo hususan udongo wa mfinyanzi huwa ni hatari sana katika kusababisha nyufa katika jengo zinazoanzia kwenye msingi. Wote tunajua kwamba msingi wa jengo ndio umeshikilia sehemu muhimu sana wa mhimili mkuu wa jengo. Sasa udongo wa mfinyanzi huwa na tabia ya kutanuka unapolowa maji au kupata unyevu kisha kukauka na kukakamaa unapopigwa na jua. Sasa udongo unapokauka unakunja msingi na kusababisha kitu kinachojulikana kitaalamu kama “shear force”, ambayo inakuwa kama inalazimisha kuuchana ule msingi wa jengo na hivyo kupelekea nyufa kwenye jengo. Lakini ikiwa eneo lina udongo wa mfinyanzi kisha baada ya kuchimba msingi ukarudishia udongo mzuri kama vile wenye mchanga zaidi basi utakuwa umeepuka changamoto hiyo ya nyufa katika jengo hilo itakayotokana na kukakamaa kwa udongo.
6. Uwepo wa miti mikubwa yenye mizizi mirefu na mipana katika eneo hilo.
Uoto kwa ujumla na hususan miti ni chanzo kimojawapo hatari sana kinachosababisha nyufa kwenye majengo. Hii ni kwa sababu mizizi ya miti kwa kawaida ina nguvu kubwa sana inapotanuka na inapokutana na msingi wa jengo chini ardhini husukuma mpaka kubomoa na hivyo kupelekea nyufa kwenye jengo husika. Ikiwa eneo lina miti mikubwa ni muhimu kuchunguza aina ya mizizi ya mti/miti husika na kama ina mizizi mikubwa inayotanuka ni muhimu kuchukua hatua mara moja na kuikata kisha kuiondoa kabisa kabla ya kuanza kujenga msingi wa jengo tarajiwa.
7. Baadhi ya mihimili au vipengele vya jengo kuruhusu kupitisha maji.
Baadhi ya vipengele vya jengo na hususan mihimili inapokuwa na vitobo vikubwa yanayoruhusu kupitisha maji hupelekea kudhoofika na kusababisha nyufa baada ya muda. Kipengele chocho cha jengo hakipaswi kuruhusu kupitisha maji. Changamoto hii huweza kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutomwagilia maji vya kutosha kwenye maeneo yenye zege wakati wa ujenzi, kukosekana kwa uwiano sahihi wa maji na saruji wakati wa ujenzi, kutoshindilia vizuri zege au kitu kingine wakati wa ujenzi na wakati mwingine hata kuzeeka sana kwa mhimili wenyewe au kipengele husika cha jengo.
8. Ujenzi ulio katika viwango dhaifu.
Ujenzi dhaifu hutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchakachua sana vifaa vya ujenzi na kupelekea kukosekana kwa uwiano sahihi, kukosekana kwa usimamizi madhubuti, kukosekana kwa maarifa sahihi ya ujenzi kwa wale wanaohusika kusimamia ujenzi huo, ujinga, uzembe na sababu nyingine nyingi zinazopelekea ujenzi dhaifu.
9. Kutofanyika kwa ukarabati wa jengo.
Kufanyika kwa ukarabati wa mara kwa mara kuhakikisha kwamba jengo liko salama mara zote hupunguza sana hatari ya kutokea kwa nyufa. Lakini pale ambapo jengo linakuwa halikaguliwi wala kufanyiwa ukarabati sambamba na kuzuia hatari mbalimbali zinazoweza kupelekea uharibifu wa jengo huwa chanzo kikubwa cha nyufa katika jengo.
10. Majanga ya asili.
Majanga mbalimbali ya asili kama vile tetemeko la ardhi, vimbunga, mvua kubwa, Dhoruba, mafuriko pamoja na mambo mengine mbalimbali ni chanzo kikuu cha nyufa katika kuta za jengo. Majanga haya mara nyingi hudhoofisha msingi na kusababisha nyufa kuendelea mpaka maeneo mengine yote ya jengo.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!