KWENYE UJENZI WEWE MTEJA UNATAKIWA KUWA NA MKADARIAJI UJENZI(QS).
Moja kati ya maeneo ambayo kumekuwa na changamoto kubwa sana katika mchakato wa mradi wa ujenzi ni katika eneo hili la kujua gharama sahihi za ujenzi. Jambo hili limekuwa linaleta changamoto na matatizo mengi kwa sababu watu kwa kushindwa kujua gharama sahihi na halisi za ujenzi wa jengo lake wamekuwa wakitumia hisia kufanya maamuzi au wakiwasikiliza watu ambao hawana ujuzi wala uzoefu wowote wa kwenye ujenzi. Hilo limekuwa linapelekea aidha migogoro kati ya mteja na wataalamu wake au kazi husika kufanyika kwa viwango duni.
Sasa suluhisho la eneo hili la kujua gharama sahihi za ujenzi kuanzia vifaa mpaka ufundi kwa mteja mwenyewe kuwa na mtaalamu wake wa ukadiriaji majenzi. Wataalamu wa ukadiriaji ujenzi au maarufu kama Quantity Surveyors(QS) ndio watu sahihi kabisa kitaalamu katika kutengeneza mahesabu ya vifaa na ufundi unaotumika kwenye ujenzi na ndio ambao huwezi kujua au kufanya makadirio sahihi ya ujenzi na kumhakikishia mteja sambamba na mkandarasi kwamba gharama hizo ni sahihi kwa mradi huo au pengine ziko juu sana au chini sana na madhara yake.
Kupata uhakika wa gharama kutoka kwa mkadiriaji ujenzi ndio kutaondoa mashaka kwa mteja na hata wataalamu wengine kwamba gharama anazopewa za ujenzi ni sahihi au la. Hii ni tofauti na kutegemea maneno ya mtaani ya kusikia au watu wa karibu wanaotumia hisia kusema kwamba hizo ni gharama kubwa au ndogo kwa sababu hawajui namna mradi unaendeshwa wala hawajui mabadiliko ya vifaa vya ujenzi ambayo hutokea mara kwa mara na kuongeza au kupunguza gharama hizi za ujenzi.
Hivyo ikiwa mtu unataka kufahamu gharama sahihi za mradi wako wa ujenzi ili uweze kufanya maamuzi sahihi ya namna ya kuuendesha mradi huo au mtu sahihi wa kumpa mradi huo kwa kuangalia beo zake, ni vyema kwanza umtafute mtaalamu wa ukadiriaji ujenzi na kumpatia michoro ya ramani za uejnzi ili aweze kufanya kazi hiyo. Baada ya kazi ya mkadiriaji ujenzi kukuonyesha uhalisia wa gharama za mradi wako sambamba na vifaa vinavyokwenda kutumika na ufundi unaokwenda kuhusika katika mradi huo, mtu unakuwa kwenye nafasi sahihi zaidi ya kuamua kwa usahihi. Kwa sababu mkadiriaji ujenzi anaweza kukupa pia tathmini ya maamuzi unayokwenda kufanya ni rahisi kuona kwa uwazi zaidi ni maamuzi gani ambayo ni sahihi kwa wewe kufanya.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!