KWENYE UJENZI USIPOKEE USHAURI AMBAO HUJAOMBA.

Kwa asili sisi binadamu tuna tabia ya kisaikolojia ya kurithi ambapo huwa tunawamaamini zaidi watu wetu wa karibu au watu ambao tuna mahusiano nao ya karibu kuliko watu wa mbali tusiowajua au kuwa na ukaribi nao. Yaani tumeumbwa kwamba wale watu ambao tuna mahusiano ya karibu na ya kina huwa tunaamini zaidi kile wanachotuambia na hata kuchukua hatua. Tabia hii ilikuwa ni jambo la msingi sana huko zama za kale lakini kwa sasa haina umuhimu mkubwa tena au ulazima kwetu. Lakini hata hivyo bado tabia hii ni tabia yenye nguvu kubwa ndani yetu kisaikolojia na mara nyingi kama tusipoweka umakini huwa tunajikuta tunaendelea kuifuata.

Jambo hili limepelekea kwamba watu wamekuwa wakichukua ushauri rahisi usiozingatia taaluma husika na wala usio na thamani kubwa ndani yake na hilo kuwagharimu sana baada ya muda mchache baadaye. Ni kweli kwamba mara nyingi watu hawa wa karibu wamekuwa wakitoa ushauri huo kwa nia njema kabisa na kwa nia ya kujenga lakini sehemu kubwa ya ushauri huo umekuwa ukihusisha zaidi hisia za mtoa ushauri au uelewa mdogo sana wa jambo na hivyo kuishia kuwa ushauri usio sahihi au wakati mwingine ushauri mbovu na unaokuja na gharama kubwa.

Kwenye taaluma ya ujenzi tabia hii haijawaacha watu salama pia, mara nyingi watu wamekuwa wakipokea ushauri ambao hata hawajauomba kutoka kwa watu wao wa karibu au ndugu, jamaa au rafiki na kwa sababu mtu wa karibu anaaminika zaidi kisaikolojia hivyo wamekuwa wakiingiza ushuri huo katika utekelezaji na kuishi kuwa ni majanga makubwa. Kuna mifano mingi ya watu ninaowafahamu binafsi waliofanya hivi na kusababisha matatizo makubwa kuliko yale yaliyokuwepo mwanzoni au kutengeneza matatizo mapya makubwa sana. Hivyo eneo hilo ni la kuweka umakini mkubwa.

Swali ni je? Ni wapi pa kupata ushauri sahihi? Kupata ushauri sahihi ambao kweli utaleta suluhisho au kuongeza thamani kwenye mradi wako unapaswa kutafuta mtu sahihi ambaye ni mtaalamu husika wa ujenzi. Na jambo la muhimu pia ni kujitahidi kulipia ushauri huo ili mhusika aweke nguvu na akili zake katika ushauri husika na kuuchukulia kwa uzito ili hata na wewe pia uuthamini ushauri huo. Ushauri wa bure kutoka kwa mtu ambaye sio mtaalamu wa ujenzi ni ushauri rahisi, na ushauri rahisi hukosa utaalamu sahihi uliozingatia kanuni na vigezo vya kitaaluma na hivyo mara nyingi huishia kwenye uharibifu zaidi au kutengeneza matatizo mapya.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *