UAMINIFU KATIKA USIMAMIZI NA UFUNDI WA UJENZI NI CHANGAMOTO KUBWA SANA.

Miradi ya ujenzi ni kati ya miradi ambayo huhusisha matumizi makubwa ya fedha ambayo huwepo katika kila kipengele cha ujenzi. Kwa sababu moja kati ya miradi inayogharimu fedha nyingi sana katika maisha ya mtu yeyote na hata serikali ni miradi ya ujenzi. Na katika hali ya kawaida sehemu yoyote yenye fedha nyingi huwa kuna nongwa kubwa na watu mbalimbali wenye malengo tofauti tofauti huingiza maslahi yao eneo hilo, kuanzia watu wadogo sana mpaka watu wakubwa kabisa.

Uwepo huu wa maslahi mbalimbali na fursa za kujinufaisha kifedha zinazoonekana kuwa zinapatikana maeneo hayo imepelekea suala la uaminifu kuadimika kwa viwango vya juu sana katika maeneo ya ujenzi. Watu wanaominika na kupewa kazi za ujenzi pia kwa sababu ya hulka ya tamaa ya kibinadamu wamekuwa wanashindwa kudhibiti hisia zao za tamaa na kupelekea kufanya udanganyifu mkubwa kwa namna za tofauti tofauti ili kupata fedha nyingi za haraka isivyostahili.

Hili limekuwa ni janga na kilio kikubwa kisichoisha katika miradi ya ujenzi kwani wateja wengi wamekuwa wakiwaamini watu kwa namna wanavyoongea huku wakiwa hawajua ni eneo gani lenye udhaifu wanalopaswa kulidhibiti ili kuzuia ubadhirifu na ukosekanaji mwingine wa uaminifu. Hata licha ya kwamba kuna njia nyingi sana za kuzuia ubadhirifu na ukosaji wa uaminifu kwa kiasi kikubwa sana lakini njia sahihi pekee ya kuzuia kukosekana kwa uaminifu ni kwa kufanya kazi na watu waaminifu. Kufanya kazi na watu waaminifu sio tu kutakuondolea kero kubwa ya kukosekana kwa uaminifu bali pia kutasaidia mradi kufanyika kwa umakini na kwa muda uliokusudiwa.

Hata hivyo pamoja na kwamba uaminifu umekuwa bidhaa hadimu sana kiasi cha watu wengi kukata tamaa kama kweli wanaweza kupata watendaji waaminifu lakini bado kuna watu wachache wenye uaminifu mkubwa katika kitu chochote wanachopewa jukumu la kukifuatilia. Wapo watu ambao aidha kwa kujua faida za mbeleni za kuwa mwaminifu au kwa kujaliwa tabia ya uaminifu kiasili wamekuwa wana uaminifu na uadilifu wa hali ya juu katika kazi. Watu wengi wenye malengo makubwa na wenye matumaini ya kufanya mambo makubwa katika maisha yao wamekuwa na msimamo mkali sana katika eneo la uaminifu katika kazi zao. Ukiweza kupata hao na kufanya nao mradi wao uwezekano wa kufanya kazi nzuri ya uhakika ni mkubwa japo wanaweza pia kuwa na masharti makali na msimamo katika namna ya utoaji wa huduma zao.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *