AINA ZA UDONGO WA KURUDISHIA KWENYE MSINGI.

Baada ya msingi wa jengo kuchimbwa na kisha kumwagwa kwa zege ya chini kabisa kwenye msingi(blinding concrete) na kujengwa kwa tofali za kwenye msingi kinachofuata huwa ni kurudishia udongo kwenye msingi kujaza yale maeneo ulipoondolewa na hakujajengwa. Zoezi la kurudishia udongo kwa lugha ya kitaalamu huitwa, “backfilling”. Lakini hata hivyo mara nyingi hutokea kwamba udongo wa eneo husika ambao ndio umechimbwa chini kwa ajili ya kupisha ujenzi wa msingi hutokea kwamba huwa haufai kurudishia kwa sababu ni udongo hatari sana kwa usalama wa nyumba au jengo linalokwenda kujengwa eneo hilo. Udongo huu hupasua msingi wa jengo na kusababisha nyufa nyingi na za hatari na hata kudhoofisha kabisa jengo.

Kuna nyumba nyingi sana ambazo msingi wa jengo umedhoofishwa na aina hii ya udongo kutokana na kujengwa na watu wasiokuwa na uelewa au umakini wa kutosha kuhakikisha udongo usiofaa haurudishwi kwenye msingi. Hilo limepelekea nyumba hizi kupiga nyufa kubwa zinazoanzia chini mpaka juu na kudhoofisha sana nyumba hiyo. Yaani hakukuwa na makosa yoyote yale kwenye ujenzi wala uzembe wala uchakachuaji wa namna yoyote ile bali tu udongo wa sehemu husika ndio haufai kabisa kurudishia kwenye msingi wa jengo. Udongo huu huwa una tabia ya kusinyaa wakati wa mvua na kisha kutanuka sana wakati wa jua unapokauka. Tabia yake hii ya kusinyaa na kukauka ndio husababisha mara kwa mara ndio hufinya msingi wa jengo na kuuachia na hivyo kupelekea msingi kukatika na kusababisha nyufa kwenye jengo.

Hivyo sasa udongo wa mfinyanzi haufai kabisa kurudishia kwenye msingi wakati wa kujenga. Badala yake kuna aina za udongo ambazo zinatakiwa kuletwa eneo la site na kurudishiwa kwenye msingi katika eneo ambalo udongo wa mfinyanzi ndio umechimbwa. Aina hizo ni pamoja na udongo wa mchanga na udongo wa tifutifu. Hizi ni aina za udongo ambazo hazina madhara kabisa kwenye msingi kwani hazishikamani na kukakamaa na kuukata msingi wa jengo na hivyo kusababisha nyufa na jengo kudhoofika. Nyumba nyingi sana kwenye maeneo yenye udongo wa mfinyanzi zimepiga nyufa na nyingine kuleta madhara makubwa kwa sababu jambo hili halikuzingatiwa.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *