KULINDWA NA SHERIA KWENYE UJENZI FANYA KAZI NA KAMPUNI KWA MKATABA EPUKA MAFUNDI.

Kisaikolojia binadamu wengi tunapenda sana urahisi, sio tu urahisi wa gharama bali hata urahisi wa michakato na urahisi wa kukamilisha jukumu husika. Kweli japo ubongo unatupeleka kwenye kutafuta urahisi kwa manufaa fulani lakini hilo mara nyingi huambatana na gharama kubwa sana. Watu wengi linapokuja suala la ujenzi mara nyingi hutafuta watu wa kawaida au mafundi wa kawaida wawafanyie kazi zao kwa kuhofia kwamba kutumia kampuni au wataalamu wenye elimu kubwa kutaongeza sana gharama ya ujenzi. Jambo hili limekuwa linapelekea watu kujiweka katika hatari kubwa sana ya kupoteza fedha au kupata hasara iliyoweza kufidiwa.

Hata hivyo japo ni kweli kwamba huenda kampuni au mtalaamu mwenye elimu kubwa anaweza kuwa na gharama kubwa kidogo ukilinganisha na mafundi wa mtaalani lakini anakuja na manufaa makubwa sana. Faida ya kwanza na muhimu sana ya kufanya kazi na kampuni au mtaalamu mwenye elimu kubwa ni kwamba kuna nafasi kubwa sana ya wewe kusaini naye mkataba ikiwa utataka, mkataba ambao utaweza kukulinda sana kisheria pale mambo yatakapokwenda tofauti na mlivyokubaliana. Mkataba wa kisheria pia unaweza kuwa na vifungu vinavyosisitiza ubora wa kazi na namna kazi inavyopaswa kuwa ambapo kampuni au mkandarasi atahakikisha anafikia viwango hivyo kwa sababu ni sharti la kisheria kwa kazi husika.

Watu wengi wanajaribu kukimbilia mafundi wa mtaani kwa sababu ya kuamini kwamba wanakwepa gharama lakini hatari ambayo wanajiingiza na hasara ambayo wanaingia aidha kwa kujua au kutokujua kwa kutokuwa na mikataba na watu wa uhakika ni kubwa kuliko hiyo ambayo wanadhani wanaikwepa. Jambo hili linawatokea watu wengi sana hasa ukizingatia kwamba sekta ya ujenzi ni kati ya maeneo ambayo wizi na udanganyifu uko kwa viwango vya juu sana. Sehemu kubwa sana ya miradi ya ujenzi hasa ambayo inatumia mafundi katika kujenga na kulipwa kidogo kuna wizi wa vifaa vya ujenzi au vyombo na hata udanganyifu pia. Kwenye ujenzi wizi umekuwa ni sehemu ya utamaduni.

Hivyo ikiwa unahitaji utulivu na kuhakikisha unapata kile unachotaka fanya kazi na kampuni hata kama sio kampuni kubwa au mtaalamu mwenye elimu kubwa ambaye mtaingia naye mkataba ambao mtaendelea kukumbushana na kukaa kwenye masharti ya mkataba wakati kazi zinaendelea kukamilishwa. Hilo litakuondolea usumbufu, kukulindia mali zako, kukuokolea muda na kukupa uhakika mkubwa wa kupata kile ulicholenga. Lakini bado gharama za kutumia kampuni kwenye ufundi badala ya fundi hazitakuwa kubwa sana kwa sababu kwanza una uhuru wa kununua vifaa mwenyewe ikiwa utataka lakini gharama za ufundi pia zinabakia kuwa maelewano huku wewe ukinufaika kwa kiasi kikubwa.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *