HAYA NDIO MAKOSA YA KIMTAZAMO KUHUSU USIMAMIZI WA UJENZI.

Kwa mujibu wa Mwalimu na Kocha wa masuala ya Uongozi ambaye pia alikuwa mchungaji zamani mmarekani John Maxwell kwenye kitabu chake cha “21 Irrefutable Laws of Leadership” alipata kusema, “Kila kitu kinakuwa au kuanguka kwa sababu ya uongozi” (Everything rises or falls on leadership). Hii ni kanuni ya asili kwamba uongozi na usimamizi wa kitu kwa ujumla ndio unaoamua kukua au kuanguka kwa jambo husika au mradi husika. Na uongozi bora na usimamizi bora ndio utakaoamua ubora wa matokeo wa jambo husika.

Changamoto ya kimtazamo ya watu wengi kwenye miradi ya ujenzi huwa ni kushindwa kuona au kutochukulia kwa uzito eneo hili la usimamizi na badala yake kuangalia moja kwa moja kwenye eneo la utekelezaji pekee. Hii ni changamoto kubwa kwa sababu baadhi ya watu kwa kuangalia utekelezaji pekee na kusahau uongozi na usimamizi wamekuwa wakifanya makosa ya kushawishi kufanya kazi na wale wanaowaona kwenye utekelezaji na kuamua kuachana na wahusika wa usimamizi wa mradi huo wa ujenzi halafu kinachotokea baada ya hapo ni kazi kuharibika, kuchelewa, kudanganywa au kuibiwa kwa vifaa vya ujenzi na mwisho mradi kuharibika na matokeo yaaliyotarajiwa kutokupatikana.

Kitu ambacho wengi wanashindwa kuelewa ni kwamba uongozi na usimamizi ndio huwa unabeba jukumu na dhamana ya kusimamia kwa weledi mradi husika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanyika kwa usahihi na ubora, kila mtu aliyeko chini ya usimamizi huo anawajibishwa kwa uzembe, uvivu na uharibifu na kila mtu kuna namna anapangiliwa kwa kuzingatia mambo mengi sana mpaka kufanikisha matokeo yanayoonekana bora. Hivyo utekelezaji ambao umeleta matokeo bora aliyoyaona hayajatokana na mtekelezaji pekee bali ni uongozi na usimamizi bora kwa ujumla ambao hao watekelezaji wanaweza kuuheshimu na kuufuata huku wakiweka pembeni nia na matamanio yao mengine yanayoweza kupelekea kuharibika kwa mradi husika.

Lakini sasa inapokuwa kwamba watekelezaji husika wako huru kuamua watakacho na hawawajibiki kwa mamlaka yoyote zaidi ya maamuzi yao wenyewe ndipo sasa wanajikuta wakifanya vitu ambavyo ni tofauti na yale yanayotegemewa. Na zaidi ya hilo ni kwamba usimamizi wa ujenzi unahusisha michakato mingi ya kitaaluma kuzingatiwa katika kufanikisha matokeo bora yanayotarajiwa. Hivyo kwa kuondoa ule usimamizi na kubaki na mtekelezaji wa kawaida pekee kuna vitu vingi vinaweza visizingatiwe au ushauri usio sahihi unaweza kutolewa kwa maslahi ya mtekelezaji lakini ukapelekea uharibifu na matokeo duni.

Hivyo ili kufanikisha kupata matokeo bora katika kazi hizi za ujenzi ni muhimu sana tena sana kuhakikisha kwamba kuna uongozi na usimamizi sahihi unaojali kuhusu ubora na unaozingatia vigezo vya kitaaluma(professionalism) ili kufanikisha matokeo bora tarajiwa. Ni muhimu kujua kwamba kuna mambo yanaweza kuharibika lakini bado yasionekane na wahusika kwa sababu ni ya kitaalamu zaidi na madhara yake yatakuja kuonekana wakati wa kuanza kulitumia jengo wakati ambao kazi ilikwisha malizika na marekebisho yake yatahitaji tena kutumia gharama kubwa ambayo inakuwa ni kama hasara kwenye mradi husika wa ujenzi kwa kushindwa tu kuzingatia mambo sahihi.

Karibu sana kwa usimamizi makini sana wa mradi wako wa ujenzi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *