AINA ZA UJENZI

  1. UJENZI WA KUTUMIA MIHIMILI YA ZEGE

Ujenzi wa kutumia mihimili ya zege ndio ujenzi maarufu na unaotumia zaidi kuliko aina nyingine za ujenzi duniani kote. Hii ni aina ya ujenzi ambapo mihimili yote ya jengo inajengwa kwa kutumia zege.

Mihimili inayolala inaitwa boriti(beams) na mihimili inayosimama wima inaitwa nguzo(columns).

Mihimili ambao ndio hubeba watu na mizigo hai inayohamishika huitwa sakafu(slabs).

Mhimili muhimu kuliko yote ni nguzo kwani zinaungana kutoka chini kabisa mpaka ghorofa ya mwisho hivyo ukiiharibu chini inaleta madhara mpaka juu na sehemu kubwa ya jengo tofauti na boriti na sakafu ambazo ukiharibu moja madhara yake ni kwa sakafu husika peke yake.

-Tunaposema zege tunamaanisha zege yenye chuma ndani ambazo zinaongeza uimara wa hiyo mihimili na zipo kwa ukubwa tofauti kadiri ya kiwango cha mihimili husika unaotokana na kiwango cha mzigo unaotakiwa kubebwa.

Jina lake kamili ni zege ya saruji yenye chuma(reinforced cement concrete au (RCC)). RCC ni zege yenye vyuma ndani. Huu muunganiko hutengeneza zege imara sana kwa utengenezaji rahisi sana.

-Ili kutengeneza zege hii kwanza hutengeneza mishikio(miundo) inayoitwa “fomuweki” ambayo ndio hupokea hicho kimiminika cha zege na kuipa umbo linalohitajika.

Kisha mtu huangalia michoro ya mhandisi mihimili ili na kupangilia hivyo vyuma kadiri ya mapendekezo ya michoro ya mhandisi ndani ya “fomuweki” hizo na kuzifungia humo kwa kutumia nyaya maalum zilizopendekezwa pia.

Baada ya kukamilisha maandalizi ya kutengeneza zege huanza kwa kuchanganya saruji, mchanga, kokoto na maji katika mashine ya kuchanganyia kisha kumwaga katika katika hizo “fomuweki” kwa kiwango kinachotakiwa.

Zege hiyo huanza kuwa ngumu baada ya masaa machache lakini huchukua kiasi cha mwezi mzima kufikia uimara wa kutosha. Kazi ya kumwagilia zege hili huendelea kila siku ili kufanikisha mchakato mzima wa uimara na ubora unaohitajika.

-Zege hizi hutengenezwa kwa viwango tofauti kadiri ya kiasi cha mchanganyiko kilichowekwa na huamua kiasi cha mzigo unaobebwa. Viko viwango mbalimbali vya zege ambavyo hufanywa kadiri ya wingi wa saruji, unene wa chuma, wingi wa mchanga na wingi na ukubwa wa kokoto.

Aina mbalimbali za mizigo inayobebwa na jengo katika kipindi cha maisha ya jengo ambayo ndio inaamua kiwango cha zege kitakachotumika.

-Mizigo Mfu: Hii ni mizigo inayotokana na jengo lenyewe, inajumuisha mifumo ya muhimili ya jengo kama vile, kuta, chuma za baraza n.k.

-Mizigo Hai: Hii ni ile mizigo inayohamishika ambayo huingizwa kwenye jengo kadiri ya matumizi ya wakati huo. Kwa mfano samani/fenicha kama vile meza, viti, vitanda, vifaa mbalimbali vya umeme n.k.

www.ujenzimakini.com

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *