KUWA MAKINI, EPUKA KUTUMIA GHARAMA KUBWA KUJENGA NYUMBA/JENGO BOVU

Na Architect N. Moshi
+2557174590

Habari Ndugu

Karibu Tuendelee Kuelimishana Zaidi Kuhusu Ujenzi Ili Kuiboresha Zaidi Dunia Ya Ujenzi

Unaweza Ku-SHARE(Kushirikisha) Ujumbe Huu Kwa Ndugu, Jamaa, Rafiki, Ili Kumwepusha Na Changamoto Hizi Kwa Namna Moja Au Nyingine Wakati Huu Au Wakati Mwingine Yatakapomkuta

Ndugu Mdau Wa Ujenzi

Haijalishi uko makini kiasi gani, pale utakapoanza ujenzi wa jengo/nyumba yako lazima utakutana na changamoto nyingi za kiufundi na za kibinadamu.

Mamlaka zinazohusika na ujenzi nchini zimeweka taratibu ambao zikifuatwa zitapunguza sana kama sio kuondoa kabisa changamoto hizi za ujenzi lakini tatizo ni kwamba taratibu hizi hazifuatwi kwa sababu kadhaa kubwa ikiwa ni gharama na mlolongo mrefu wa kupata kibali cha ujenzi ambao unachukua muda na saa nyingine mwishoni unaweza kushindwa kukidhi masharti yao, hivyo kazi nyingi bado zinafanyika kienyeji katika kukwepa gharama na milolongo/urasimu uliokuwepo.

Hapa kwenye miradi kufanyika kienyeji ndio nataka tupaangizie kwa kuwa ndio shida kubwa ilipo inayosababisha hasara na maumivu makubwa yasiyotarajiwa. Huwa inaumiza sana mtu anapoingia gharama kubwa kujenga nyumba/jengo lakini matokeo ya mwisho yanakuwa mabovu sana kuanzia kwenye uimara, ubora na hata mvuto wa jengo husika huku akiwa ameshapoteza pesa nyingi kwa sababu tuu ya kushindwa kufanya maamuzi sahihi mwanzoni.

Kuja kufanya marekebisho ni gharama nyingine kubwa ya fedha, muda na bado mara nyingi ni vigumu kufikia ubora uliokusudiwa mwanzoni kutoka kwenye uharibifu uliofanyika.

Mambo Ya Kuzingatia Kukabiliana Na Hali Hizo.

-Mtaalamu wa ujenzi Msanifu/Mhandisi ndio watu wenye uelewa wa juu kabisa wa ujenzi(professionals), ni vyema ukamshirikisha zile hatua muhimu, kama wakati wa kujenga kwa kuanza na kukagua michoro mwanzoni na kuijadili mpaka kuridhiwa na pande zote tatu kabla ya ujenzi kuanza.

Baada ya hapo mtaalamu atahusika katika hatua ya kwanza ya setting out kabla ya msingi.
Atarudi baadaye wakati wa kujenga tofali kukagua mipangilio na ubora wa ufundi.
Kisha mwishoni kufanya ukaguzi kuhakikisha kila kitu kimefanyika kama kilivyokusudiwa.

Pia itakuwa ni jukumu lake kila inapotokea changamoto iwe ni ya kiufundi au kutoka kwenye mamlaka za ujenzi atashirikishwa katika kuitolea maamuzi. Hii itasaidia kuepusha uchakachuaji wa mafundi na kuhakikisha ubora na usalama wa kazi muda wote.

Ubora Wa Mafundi

-Hili limekuwa ni changamoto sugu kwenye miradi inayofanyika kienyeji. Kazi nyingi hazina ubora japo zinaweza kuwa imara. Pesa inayotumika kununua vifaa vya ujenzi ni nyingi sana lakini ufundi unaotumika ni duni hivyo nyumba inagharamiwa pesa nyingi lakini thamani ya pesa hiyo haionekani. Unakuta nguzo zimepinda, beam zina mawimbi, nyumba ni fupi, madirisha yanakosa mpangilio mzuri au madogo sana n.k., pesa imekwenda nyingi lakini jengo ni la hovyo. Hapa shida kubwa huwa ni mafundi wabovu.

Uaminifu wa Mafundi

-Mara nyingi inatokea kwamba mafundi wanakutajia bei ndogo ili wapate kazi au wewe unawalazimisha bei ndogo bila wewe kujua wanakubali wakijua wazi kabisa kazi hawataiweza kwa kiasi hicho lakini kwa kuwa wana shida sana ya pesa kwa wakati huo wanakubali ili wapate tu pesa angalau mwanzoni, hivyo aidha watafanya kazi mbovu sana kwa taabu au wataiachia njiani na kukimbia na wewe kuingia gharama zaidi huku wao wameshapata angalau pesa kidogo waliyokuwa wanaitamani ambayo walihofia wasingeipata endapo wangekulazimisha uwape pesa wanayoitaka.

Changamoto nyingine kwenye uaminifu ni uchakachuaji unaofanywa na mafundi ili kupunguza baadhi ya vitu au kupunguza ukubwa wa jengo kwa faida yao bila wewe kujua, na mbaya zaidi ni hata kuiba vifaa kama hakuna usimamizi mzuri.

Unamjuaje Fundi Bora Na Mwaminifu?

Changamoto ni kwamba hata fundi bora wakati mwingine anafanya kazi mbovu kwa sababu ya tamaa, shida ya pesa au kukosa umakini kwenye makubaliano.

Hivyo unahitaji fundi bora, mwaminifu na wa uhakika.
Watu ambao tumefanya kazi na mafundi wengi mbalimbali kwa muda mrefu tuna uzoefu na tabia mbalimbali za mafundi, uwezo, uimara na udhaifu wao, tunaweza kujua yupi anafaa wapi na udhaifu wake uko eneo gani

NOTE: Kitakachokufanya Uwe Na Nyumba/Jengo Bovu Kwa Gharama Ile Ile Ya Kujenga Jengo Lenye Ubora, Ni Kushindwa Kufanya Maamuzi Sahihi Mapema

Ahsante na karibu sana.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *