NAMNA YA KUJUA GHARAMA SAHIHI ZA MICHORO YA RAMANI

Suala la kujua namna ya kudadavua gharama sahihi za michoro ya ramani ya jengo limekuwa ni jambo lenye mivutano mara nyingi na kupelekea pande mbili baina ya mteja na mtoa huduma ya kutaalamu ambapo kila mmoja kuona kama hajatendewa haki. Mteja huona amefanyiwa gharama kubwa sana huku mtoa huduma ya kitaalamu kuona amepunjwa sana na changamoto hii wakati mwingine inachangia huduma husika kutokuwa katika viwango sahihi.

Kujua gharama sahihi za kitaalamu kunasaidia kila upande kuridhika

Namna ya kujua gharama za michoro kwanza tuanzie kwenye bei zilizopangwa na mamlaka husika:

-Mamlaka zilizopewa dhamana ya kujihusisha na shughuli zote za ujenzi kwa maana ya bodi za kitaaluma zinazohusika na ujenzi ndizo hukaa na kuja na mahesabu yote ya namna ya kujua viwango sahihi vya gharama kwa kila mradi na kila hatua.

-Mamlaka husika zimeweka viwango kwamba gharama zote za kitaalamu kwa ujumla kwa maana ya michoro ya aina zote na usimamizi wote wa jengo kuhakikisha limefikia viwango vinavyokubalika ni asilimia 12% ya gharama zote za kujenga jengo lote mpaka kukamilisha. Lakini katika gharama hizi gharama za kisanifu za jengo kwa maana ya kuchora ramani na kusimamia ujenzi sahihi wa ramani husika ni asilimia 6%. Hapa inamaanisha umeondoa gharama za michoro ya nondo(structural engineering drawings), gharama za makadirio ya ujenzi(quantity surveyors, BOQ), gharama za michoro ya umeme, mifumo ya majitaka n.k.,

MAMLAKA HUSIKA HUWEKA NDIO HUPANGA VIWANGO SAHIHI VYA GHARAMA ZA UJENZI

-Hivyo gharama za kuchora ramani pamoja na kusimamia ujenzi wote mpaka jengo linakamilika kwa maana ya (pre-contract and post-contract consultancy architectural services) inagharimu asilimia 6% ya gharama za kujenga jengo lote mpaka kukamilika. Sasa kutokea hapo gharama ya ramani peke yake pamoja na ushauri wote wa kitaalamu kabla ya ujenzi kuanzia ni theluthi moja ya gharama za kitaalamu kwa kazi yote, kwa maana ya kwamba ni theluthi moja ya asilimia 6% ambayo ni asilimia asilimia 2%.

ASILIMIA 2% NI GHARAMA SAHIHI NA RASMI LAKINI ASIMILIA 1% INAWEZA KUWA SAHIHI ZAIDI KAMA BEI YA MTAANI

-Sasa hii asilimia 2% ni gharama rasmi ambayo imepatikana kutokana na viwango vilivyopangwa na mamlaka za ujenzi kwa maana ya kwamba miradi yote ya serikali, taasisi za umma na taasisi binafasi pamoja na miradi ya watu binafsi hii ndio njia sahihi za kujua. Lakini sasa kwa kuwa hizi ni gharama rasmi zilizopangwa na mamlaka husika lakini kwa bei za mitaani bado inaonekana ni gharama kubwa hasa kwa watu binafsi ambao wengi hawana uwezo mkubwa au pesa ya pamoja ya kufanya mradi mzima kwa pamoja, badala yake wanafanya taratibu. Hivyo sasa kwa bei ya mtaani tunaweza kusema asilimia 1% ya gharama za kujenga jengo zima bado inaweza kuwa ni gharama sahihi kutumia kwa huduma ya michoro ya ramani ya jengo na huduma nyingine zote za kabla ya kuanza ujenzi. Kama ukiamua kuendelea kushushana sasa hapo ni makubaliano yenu lakini kiwango cha asilimia 1% ni kipimo kizuri cha kuona kama gharama unayotajiwa ni sahihi au la.

UNAWEZA KUTAFUTA “GOOGLE” KUJUA WASTANI WA KUJENGA MITA MOJA ZA MRABA KWA TANZANIA

-Sasa swali linalokuja ni namna ya kujua gharama sahihi za kujenga jengo lote mpaka kukamilisha. Kujua gharama za kujenga jengo lote mpaka kukamilisha inatakiwa kwanza ujue gharama za kujenga mita moja ya mraba kisha utachukua mita za mraba za jengo zima kisha utazidisha kwa gharama za kujenga mita moja ya mraba na hapo utapata gharama za kujenga jengo lote mpaka kukamilisha. Baada ya kupata gharama za jengo lote ndio kisha utadadavua asilimia % husika na kujua gharama hiyo. Gharama za kujenga mita moja ya mraba za jengo au kwa kiingereza (1 square metre) zinapangwa na mamlaka husika yaani bodi za kitaaluma za ujenzi. Ukiingia kwenye website zao wameweka gharama hizo au ukiuliza wahusika au wataalamu wanaohusika watakujulisha au unaweza ku-google “construction costs per square metres in Tanzania” na utapata gharama sahihi kwa mita mja za mraba. Gharama hizi pia hubadilika kadiri ya mabadiliko ya vifaa vya ujenzi mitaani pamoja na mifumuko ya bei kwenye uchumi(inflation) hivyo huwa hazibaki vile vile miaka yote.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *