NYUMBA YAKO INAHITAJI UKARABATI

Kwenye fizikia kuna dhana moja inayoitwa “entropy” ambayo ni kama kanuni inayomaanisha kila kitu kilichopo duniani huwa kinaenda kikipoteza thamani yake taratibu kadiri muda unavyokwenda mbele.

Sasa kutokana na nyumba kuchukua muda mrefu ukilinganisha na vitu vingine kabla ya kuanza kupoteza thamani yake basi baada ya kumaliza kujenga ni wachache ambao huendelea kufikiri kwamba watahitaji kufanya ukarabati baada ya miaka kadhaa. Hili limepelekea watu wengi kuendelea kuishi kwenye nyumba zisizo za hadhi yao kwa kutokuwa na wazo hilo katika akili zao.

Sambamba na sababu hizo za ubora kuporomoka zifuatazo ni sababu kwa nini nyumba yako inahitaji ukarabati ambao wakati mwingine utajumuisha hata mabadiliko ya kimwonekano na matumizi ya ndani.

UKARABATI UNAWEZA KUJUMUISHA MABADILIKO YA KIMUONEKANO NA KIMATUMIZI

(i) Hadhi ya nyumba yako inashuka na ubora wake kuporomoka; Kila mtu anafahamu kwamba kila kitu anachotumia kwenye maisha yake kinashuka hadhi yake na ubora wake kuporomoka kadiri muda unavyoendelea kwenda mbele iwe ni nguo, viatu, simu, tv, kompyuta, fridge, kitanda, gari, shuka na hata vifaa vya kazi. Kupotea huku kwa ubora na kushuka hadhi yake hupelekea mtu aidha kununua kingine au kuboresha kilichopo au kufanya vyote viwili kutegemea na mahitaji yake. Nyumba nayo kama kitu kingine chochote hupungua hadhi yake na ubora wake kuporomoka hivyo nayo baada ya miaka kuanzia 10, 15 mpaka 20 huhitaji ukarabati ili kuiboresha upya, kuiongezea thamani na kuipandisha hadhi yake tena ili kukupa wewe mtumiaji thamani unayostahili.

UKARABATI UNAONGEZA THAMNI NA HADHI YA JENGO

(ii) Inapitwa na wakati; Sisi binadamu ni viumbe ambao tunapenda kwenda na staili tofauti zilizo kwenye wakati na sio watu wa kukubali kuachwa nyuma, asili hii hutufanya pale tunapokaa na kitu cha staili ya zamani muda mrefu huku kuna stili mpya zilizoboreshwa zaidi na zinazokubalika zaidi basi kile cha zamani huanza kutuletea karaha, kuonekana kero na kutunyima raha ambapo ili kuondoa kero hiyo tunahitaji kufanya mabadiliko ambayo yataongeza ubora, thamani na kutuongezea hadhi kwenye jamii tunayoishi. Kufanya ukarabati na kuongeza ubora kutatuongezea hadhi tunayostahili.

MAMBO HUPITWA NA WAKATI

(iii)Kipato chako kinaongezeka: Mara nyingi kadiri muda unavyoendelea mbele kipato huwa nacho kinaongezeka, iwe mtu anamiliki biashara, biashara hiyo hukua kutokana na uelewa wake na maarifa yake kwenye biashara husika kuongezeka sana au kama mtu ni mwajiriwa uzoefu na maarifa yake kwenye ajira husika hukua sana na hivyo kuongeza kipato chake. Sasa mara nyingi wakati unafanya ujenzi wa nyumba hiyo mwanzo kipato kilikuwa kidogo na maamuzi mengi ulifanya kadiri ya uwezo wako, sasa hivi una kipato kikubwa na unaona kwamba ungekuwa unajenga sasa kuna vitu vingi ungefanya kwa utofauti na ubora zaidi, sasa kwa sababu hiyo unahitaji kufanya ukarabati ili yote unayotamani kwa sasa yaboreshwe kwenye nyumba yako ili ikuongezee hadhi unayoistahili inayoendana na uwezo wako wa sasa kifedha.

UKARABATI UNAONGEZA NA KUBORESHA VITU VINGI

(iv)Mabadiliko ya teknolojia: Dunia inakwenda kasi sana na mambo mengi yanabadilika kwa kasi sasa, Kuna mambo hukuyazingatia wakati unajenga nyumba yako kwa mara ya kwanza lakini sasa hivi unayahitaji kwenye nyumba yako, hivyo unahitaji kufanya ukarabati ili kuyajumuisha huko.

MABADILIKO YA TEKNOLOJIA YANAPELEKEA MABADILIKO YA BAADHI YA VITU NDANI YA JENGO

(v)Kubadilika kwa matumizi: Mawazo yetu siku zote huwa yanabadilika na hayajawahi kubaki kama yalivyokuwa siku za nyuma lakini pia maisha yanabadilika, hivyo mambo uliyokuwa unayahitaji miaka mitano iliyopita sio mambo utakayokuwa unayahitaji miaka mitano ijayo. Wakati unajenga nyumba yako kwa mara ya kwanza inawezekana kuna vitu ulikuwa unahitaji kulingana na mahitaji yako ya wakati huo lakini kwa sasa huvihitaji tena na kuna vitu hukuwa unavihitaji lakini sasa unavihitaji ndani ya nyumba yako, hivyo utahitaji kubadili matumizi ya baadhi ya nyumba au kuongeza ukubwa au nyumba yenyewe na hivyo utahitaji ukarabati.

MAWAZO YETU HUENDELEA KUBADILIKA KILA MARA NA KUPATA MAWAZO BORA ZAIDI

(vi)Kurekebisha makosa: Watu wengi sana hufanya makosa wakati wa kujenga nyumba lakini huja kugundua makosa hayo baadaye wakati tayari wanaishi ndani ya nyumba hiyo. Hivyo baada ya miaka kadhaa kupita wanahitaji kuja kufanya ukarabati ili kurekebisha makosa hayo.

MTUMIAJI HUENDELEA KUVUTIA NA MAWAZO MAPYA NA YALIYO BORA ZAIDI

(vii)Kutambua uzuri na mvuto wa nyumba; Watu wengi baada ya kusafiri maeneo mengi tofauti tofauti hukutana na aina mbalimbali za stailia ambazo hawakuwa wanazifahamu kabla ambazo huwavutia sana na hivyo kuzitamani hivyo huhitajika kufanya ukarabati wa nyumba utakawapatia kila wanachotamani kukifanikisha.

NOTE: Ukiona umefikia mahali na kuona kwamba unahitaji kufanya ukarabati wa jengo/nyumba yako, uko sahihi kabisa lakini hatua ya kwanza ya kuchukua ni kutafuta mtaalamu wa ubunifu majengo(Architect) na kumwonyesha kile unachotaka kukifanikisha na mtaanza kujadili namna ya kufanikisha hilo.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *