SIFA ZA RAMANI SAHIHI YA JENGO
Wateja wengi wamekuwa wanakutana na changamoto sana linapokuja suala la ramani iliyokidhi vigezo vya kuitwa ramani bora ya jengo au ramani sahihi ya jengo na kwa sababu wateja wengi ni watu wasio na uzoefu kwenye fani hizi za usanifu na uhandisi basi sio rahisi kuona makosa yanayokuwepo kwenye ramani hizi mpaka jengo linapohamiwa ndipo huja kuona kwamba kuna makossa yalifanyika. Sahihi twende tuangalie ni vigezi gani vinaifanya ramani ya jengo kuwa bora na sahihi kwa mteja husika.
-Ukubwa sahihi wa vyumba na nafasi nyingine: Ramani ya jengo yenye ubora inapaswa kuwa na vyumba vyenye ukubwa unaoendana na kile kinachofanyika katika chumba husika, japo mara nyingi ukubwa unategemea na uwezo wa mteja kujenga lakini kuna viwango ambavyo chumba hakitakiwi kuzidi au kupungua ili kuweza kufaa kwa matumizi yaliyolengwa ya chumba husika au nafasi husika kama vile korido.
-Matumizi ya nishati: Ramani ya jengo yenye ubora inapaswa kuzingatia kwamba kunakuwa na mifumo ya asili ya kuingiza mwanga na hewa vya kutosha ndani ya jengo na hivyo kupunguza matumizi makubwa ya nishati katika jengo yanayolenga kuleta mwanga na hewa ndani ya jengo. Inafaa zaidi kila chumba au nafasi nyingine inatakiwa kuwa na angalau madirisha mawili au maeneo mawili ya wazi ya kuingiza hewa ndani ya chumba husika ili kusaidia hewa kuw ana pa kuingilia na pa kutokea kitu kinachofanya chumba husika muda wote kuwa na hewa safi inayozunguka.
-Uzuri wa muonekano: Jengo ni kitu ambacho kiko wazi na huwezi kukificha, kila anayepita analiona na kuhukumu kadiri ya jinsi lilivyomvutia, hata hivyo japo tunaamini kwamba kila mtu ana tafsiri na mtazamo wake binafsi juu ya uzuri wa kitu lakini kuna kanuni maalum za kuzingatia ambazo hazibadiliki na zilizokubalika ambazo zikitumika zinaleta tafsiri inayokubalika ya uzuri wa kitu kama vile usawa na upacha. Hivyo jengo lolote linapaswa kuzingatia kanuni fulani zinazolipa tafsiri sahihi ya uzuri kwani linapokuwa katika viwango bora vya uzuri wa kimuonekano litavutia sana watu na kuleta hamasa ya watu wengi kujitahidi kufikia viwango bora kwa majengo mengine yatakayofuata.
-Kujengeka: Ramani sahihi ya jengo inapaswa iwe imefanyika kwa namna ambayo inajengeka badala ya kuwa na “mbwembwe” nyingi lakini unapokuja kwenye uhalisia unakuta ni kitu kisichofaa kujenga kwa sababu aidha ya teknolojia hiyo ya ujenzi kuwa juu sana ya viwango au wakati mwingine bajeti kutokuweza kuhimili gharama za mapendekezo husika.
– Uwiano sahihi wa vyumba na kimo: Ramani sahihi ya jengo inapaswa kuzingatia uwiano sahihi wa vyumba kwa maana ya kwamba kama una sebule yenye ukubwa wa mita za mraba 50, basi hatutegemei uwe na vyumba vyenye ukubwa wa mita za mraba 7, au kama una chumba chenye ukubwa wa mita za mradi 30 hatutegemei chumba hicho kiwe na bafu lenye mita za mraba 2 badala yake kunatakiwa kuwe na uwiano unaoendana wa ukubwa huu wa vyumba na nafasi nyingine ndani ya jengo.
-Uelekeo sahihi: Ramani sahihi ya jengo inapaswa kukaa kwenye uelekeo sahihi katika eneo jengo linapojengwa, kwa maana ya kwamba mtu unapaswa kufika site na kufahamu maeneo ya jirani, barabara, uelekeo wa upepo, uelekeo wa jua, upande bahari, ziwa au mlima ulipo n.k., hivyo kuamua kwa usahihi ni wapi jengo linapaswa kutazama na kwa sababu gani.
-Mpangilio sahihi wa vyumba na mzunguko wa ndani: Ramani sahihi ya jengo inapaswa kuzingatia sana mpangilio wa vyumba na nafasi nyingine ndani ya jengo kadiri ya matumizi na utamaduni wa mteja husika. Kwa mfano ni wazi kwamba sehemu ya jiko inapaswa kuwa karibu na eneo la kulia chakula(dining) kutokana na mahusiano yaliyopo kati ya maeneo haya mawili, ngazi nazo zina sehemu yake sahihi ya kukaa, maliwato ya umma nayo yanapaswa kuwa na faragha ya kutosha, mpangilio wa vyumba unapaswa kuzingatia faragha kadiri ya matumizi yake, milango ya kuingilia na kutoka ndani ya jengo inapaswa kuzingatia mapendekezo ya mteja pia, jiko linapaswa kuwa na stoo yake na veranda pamoja na mlango wa nyuma kutokana na aina ya matumizi yenyewe n.k.,
-Kuendana na viwango vilivyowekwa na mamlaka husika: Ramani sahihi ya ujenzi inapaswa kuzingatia na kukidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika ili kuepusha usumbufu na kuingia kwenye mivutano na mamlaka hizi wakati wa ujenzi ambapo inaweza kuathiri kazi, kuleta hasara kubwa na hata kupoteza fedha kutokana na kupigwa faini mbalimbali za kukiuka taratibu zilizowekwa.
-Kuwa na mahitaji yote muhimu: Ramani sahihi ya ujenzi inapaswa kuzingatia mahitaji yote muhimu ya ndani ya jengo kwa maana ya kwamba kama sehemu inahitaji maliwato inatakiwa iwepo, kama kunahitajika stoo inapaswa iwepo kwani vitu hivi huja kuleta usumbufu mkubwa baadaye pale vinapohitajika kutumika lakini havikuwekwa.
-Upatikanaji wa malighafi zilizopendekezwa: Ramani sahihi ya ujenzi inapaswa kuwa imependekeza malighafi zinazoweza kupatikana ili kukamilisha ujenzi husika. Itakuwa haina maana kama ramani imefanyika vizuri lakini inafikia mahali inakwama kwa sababu malighafi iliyopendekezwa kwenye michoro haiwezi kupatikana.
-Kuzingatia mahitaji na mapendekezo ya mteja: Ramani sahihi ya ujenzi inapaswa kuzingatia mahitaji na mapendekezo yote ya mteja kwani yeye ndiye mlengwa mkuu na wakati mwingine mtumiaji wa jengo husika. Kwa yale ambayo kitaalamu hayawezekani yanaweza kutafutiwa mbadala wake au mteja kushuariwa kwa usahihi lakini mwisho wa siku mteja anapaswa kuwa ameridhika na kile kilichofanyika.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!