MICHORO YA RAMANI YA USANIFU WA JENGO(ARCHITECTURAL DRAWINGS)

Huduma ya ushauri wa kitaalamu ambayo hufanyika kabla ya kuanza ujenzi hujumuisha michoro ya ramani ya usanifu wa jengo pamoja na michoro mingine ambao ndio hukabidhiwa tayari kwa kutoa mwongozo wa kuanza kujenga nyumba. File hili la michoro ya ramani ya usanifu wa jengo hujumuisha set 6 mpaka 7 za michoro hii ya “architectural” kama ifuatavyo.

Mchoro wa ramani ya kiwanja(site plan): Hii ni aina ya kwanza ya michoro ya usanifu wa jengo ambayo inaonyesha ramani ya kiwanja, sehemu ya kiwanja ambapo nyumba itajengwa, geti la kuingilia nyumbani lilipo, barabara inapopita na njia za ndani ya kiwanja, eneo la parking ya gari, eneo la bustani, miti na maua, mfumo wa majitaka na mabomba ya maji machafu sambamba na mashimo yanapokaa, ukubwa wa kiwanja na uwiano wa nyumba na kiwanja chenyewe, upande ambapo nyumba inatazama, pamoja na majengo mengine na vitu vingine vilivyopo kwenye kiwanja tofauti na nyumba kubwa yenyewe kama vile swimming pool, nyumba ya ziada(servant quarter) n.k.,

MCHORO WA RAMANI YA JENGO

Mchoro wa ramani ya sakafu ya chini ya jengo(floor plan): Hii ni aina ya pili ya michoro ya usanifu wa jengo ambayo inaonyesha mpangilio wa vyumba ndani ya jengo, vipimo vya ukubwa wa kila chumba na baraza zilizopo pamoja na nafasi nyingine za ndani, milango yote ya nje na ndani ya jengo na vipimo vyake, madirisha yote jengo, mpangilio wa samani za ndani ya jengo(furnitures) na uwiano wake na vyumba husika pamoja na majina ya kila eneo la nyumba.

MCHORO WA RAMANI YA SAKAFU YA CHINI YA JENGO

Michoro ya muonekano wa pande za jengo(Elevations): Hii ni aina ya tatu ya michoro ya usanifu wa jengo inayoonyesha pande za jengo kwa muonekano kwa maana ya upande wa mbele wa jengo(front elevation), upande wa nyumba(rear elevation), upande wa kushoto(left side elevation) pamoja na upande wa kulia wa jengo(right side elevation).

MICHORO YA MUONEKANO WA PANDE ZA JENGO

Mchoro unaolikata jengo katikati(Cross section): Hii ni aina ya nne ya michoro ya usanifu wa jengo ambayo inaonyesha vielelezo muhimu za maeneo ya ndani ya jengo kama vile aina ya malighafi iliyopendekezwa kuanzia kwenye msingi mpaka kwenye paa, sambamba na kuonyesha kimo cha jengo kuelekea juu(vertical height) ikiwa ni pamoja na kimo cha milango kwenda juu, kimo cha madirisha kwenda juu, kimo cha msingi, kimo cha paa, kimo cha kuta, kimo cha “lenta” na nafasi zilizoko kwenye eneo mchoro huo ulipokatwa katika ramani ya sakafu ya jengo.

MCHORO UNAOLIKATA JENGO KATIKATI

Mchoro wa ramani ya paa(Roof plan): Hii ni aina ya tano ya mchoro ambayo inaonyesha ramani na muundo wa paa la jengo husika pamoja na vielelezo vya malighafi zilizopendekezwa kwenye paa husika.

MCHORO WA RAMANI YA PAA LA JENGO

Picha za muonekano wa jengo(3D’s Perspectives): Hii ni aina ya sita ambayo inaonyesha muonekano wa wa jengo litakavyokuwa pale litakapokuwa limemalizika kujengwa endapo litajengwa kama jinsi lilivyochorwa.

PICHA YA MUONEKANO WA JENGO LITAKAVYOKUWA LIKIMALIZIKA

Michoro ya mifumo ya majitaka(Septic details): Hii ni aina ya saba ya michoro ambayo huonyesha vielezo muhimu pamoja na vipimo vya mifumo ya majitaka nje ya jengo.

MICHORO YA MIFUMO YA MAJITAKA

NB: Hii ni michoro ya usanifu wa jengo(architectural drawings), ambayo inatosha kwa nyumba za kawaida peke yake, lakini kutegemea na aina ya jengo na matumizi ya jengo kuna michoro mingine huhitajika ya kuongezea kama vile michoro ya uhandisi mihimili(structural engineering drawings), michoro ya uhandisi umeme, michoro ya uhandisi huduma(service engineering drawings) n.k., hata hivyo michoro ya usanifu wa jengo ndio hutangulia na ndio huamua namna hiyo michoro mingine itakavyokuwa.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *