KUFANIKISHA UJENZI BORA EPUKA KUTUMIA HISIA, ANGALIA MANUFAA.

Mara nyingi sisi binadamu tuna udhaifu wa kuongozwa na hisia zaidi na kutoona uhalisia jambo linalopelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi mara nyingi zaidi kuliko maamuzi sahihi na mwishoni tunaishia kujutia na kusema laiti ningejua, watu wachache ambao wamejaliwa kutumia akili na maarifa zaidi kuliko hisia wamekuwa wanashinda zaidi kuliko wengi wanaoongozwa na hisia. Changamoto ni kwamba ukishatawaliwa na hisia huwa husikii wala huoni, ni baada ya kuumia na kujutia ndio hisia huondoka na uhalisia kuja kukuonyesha kwamba hukutakiwa kufanya hivi bali vile.

  • Linapokuja suala la ujenzi kwa kuwa huwa linahusisha fedha nyingi basi hisia huchukua nafasi kubwa zaidi kuliko uhalisia na mara nyingi kuongozwa huku kwa hisia hakuwaachi watu salama, kila mtu huishia na majuto yake peke yake. Hivyo ni vyema kila unapojishughulisha na ujenzi ambao unahusisha fedha nyingi jaribu kukazana kuangalia manufaa zaidi badala ya kuongozwa na hisia kama za tamaa au urahisi wa kufanikisha vitu.

Katika ujenzi maamuzi ya nani wa kumpa kazi yanapotakiwa kufanyika watu badala ya kuangalia ubora, uwezo na uzoefu wa mhusika hukimbilia kuangalia yule aliyetaja bei ndogo na kumpa kazi kwa sababu anaangalia urahisi wa kukamilisha kazi lakini mara nyingi unakuja kukuta kwamba yule wa bei ndogo labda anafanya kazi taratibu sana pengine mara tatu ya muda ambao mwingine anaweza kufanya kwa bei ya juu zaidi, au anafanya kazi ya viwango vya chini sana kiasi kwamba itaanza kuhitaji ukarabati mkubwa na wa gharama zaidi miaka michache baadaye, au wakati mwingine utakuta huduma nyingine zinazofuatia zitapelekea gharama kubwa sana kuziba ubovu wa kazi iliyofanyika kwa bei ndogo.

MAAMUZI YANAYOHUSISHA FEDHA NYINGI HUATHIRIWA SANA NA HISIA

Katika kufanya maamuzi ya ununuzi wa malighafi za ujenzi napo hisia pia huingia na mtu kukimbilia vitu vya gharama ya chini kwa mfano matofali ya bei ndogo zaidi ambayo ni dhaifu sana kwa sababu saruji imechakachuliwa sana ndio maana yakauzwa kwa bei ndogo au mabati ambayo ni mepesi sana ndio maana yakauzwa kwa bei ndogo lakini yanakuwa na maisha mafupi sana yasiyolingana hata na bei yake kwa wastani.

MALIGHAFI YA BEI RAHISI MARA NYINGI HUWA NA MAISHA MAFUPI

Hivyo kuepuka kutumia hisia hasa za tamaa na urahisi kutakuwa na manufaa mkaubwa kwako kuliko unavyoweza kufikiria na unaweza kuja kujua manufaa hayo angalau kidogo baada ya kuwa umeamua na kujutia kwa kusema laiti ningejua. Fanya maamuzi sahihi yasiyoongozwa na hisia na utakuja kujishukuru baadaye.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *