JENGO SAHIHI LINAPASWA KUWA NA HEWA NA MWANGA ASILI VYA KUTOSHA NDANI YA JENGO.

Bado imekuwa ni changamoto sana kwa watu kujua hasa ni vigezo gani vinalifanya jengo kuwa sahihi zaidi kitaalamu kadiri ya umahiri na ubora wa msanifu wa jengo, japo wakati mwingine hili linategemea na malengo ya matumizi ya jengo husika lakini kwa ujumla kuna vigezo ambavyo mara nyingi ni muhimu katika kulikamilisha jengo kuitwa ni jengo sahihi au (intelligent building).

Moja ya vigezo hivi ni jengo kuweza kuingiza hewa na mwanga wa kutosha ndani ya jengo, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa litapelekea kupunguza matumizi makubwa ya nishati yanayohitajika kuleta mwanga na hewa asili ikiwa usanifu wa jengo haujazingatia haya kwa namna moja au nyingine.

KUWA NA UWAZI WA HEWA KUINGIA NA KUTOKA NDANI YA JENGO

Japo ni kweli kwamba sio rahisi kufanikisha kuweka kila kitu kwa asilimia 100% hasa kwa majengo makubwa ambayo yanahitajika kuwa na vyumba na nafasi nyingi ndani ya jengo lakini bado ziko mbinu nyingi za kuhakikisha hili linafanikiwa kwani lina manufaa makubwa.

MBINU NYINGI ZINATAKIWA KUTUMIKA KUHAKIKISHA MWANGA ASILI NA HEWA ASILI VINAZINGATIWA NDANI YA JENGO

Kwa mfano chumba chochote hasa kwenye nyumba za kuishi kinatakiwa kuwa na angalau sehemu mbili zenye uwazi(openings) au madirisha angalau mawili ili kusaidia mzunguko sahihi wa hewa ndani ya chumba ambao utahakikisha muda wote chumba kinakuwa na hewa safi kwa sababu hewa inapata nafasi ya kuingia na kutoka muda wote hivyo kukifanya chumba kuwa na utulivu na faraja ya kipekee, bila usumbufu wala kelele. Lakini pia wingi wa sehemu zenye uwazi unaongeza mwanga wa kutosha ndani ya jengo ambapo muda mwingi jengo litakuwa na mwanga bila kutegemea taa zinazotumia nishati mbadala kama umeme, mafuta n.k,.

CHUMBA KINAPASWA KUWA NA SEHEMU ZENYE UWAZI(OPENINGS) ANGALAU MBILI KWA AJILI YA MZUNGUKO WA HEWA KUINGIA NA KUTOKA NDANI YA JENGO

Jengo linapokosa mwanga wa kutosha na hewa asili ya kutosha hulazimika kutumia nishati mbadala kama vile umeme kwa wingi sana ili kuwasha taa za kuleta mwanga wa kutosha ndani ya jengo au kuwasha kiyoyozi (air condition), ili kulazimisha hewa safi ndani ya jengo.

JENGO LINAPOKOSA MWANGA AU HEWA YA KUTOSHA LINALAZIMIKA KUTUMIA NISHATI MBADALA

Hata hivyo mwanga asili na hewa asili licha ya kwamba vinapatikana bure bila kuhusisha gharama kubwa ya nishati lakini pia vina uasili ambao ni bora kuliko mwanga na hewa vinavyoletwa na nishati na hata kiafya mwanga asili na hewa asili havina madhara kama ilivyo kwa kiyoyozi ambacho huja na madhara kiasi kiafya.

MWANGA NA HEWA ASILI HAVINA MADHARA KIAFYA KAMA ILIVYO KIYOYOZI INAYOPATIKANA KUPITIA NISHATI MBADALA

Jengo linalotegemea nishati katika kuwasha vitu hivi linaongeza gharama kubwa zaidi kwa watumiaji wa jengo kuliko lile ambalo limezingatia kuhakikisha vitu hivi vinapatikana kwa njia za asili, hivyo unapokuwa unakutana na mtaalamu wa jengo ni vyema kuzingatia kwamba kati ya vigezo vya kuzingatia katika kufanikisha kujenga jengo sahihi ni pamoja na upatikanaji wa mwanga na hewa asili ndani ya jengo muda mwingi zaidi ukiachana na nyakati ambazo utalazimika kutumia nishati mbadala, hata hivyo kutokana na changamoto mbalimbali za kitaalamu sio mara zote unaweza kufanikisha hili kutegemea na aina, matumizi, mazingira na hata ukubwa wa mradi husika lakini kama ukizingatia hili bado itasaidia sana kukupunguzia ukubwa wa matatizo yatakayotokana na kupuuza eneo hili.

MWANGA NA HEWA ASILI VINAOKOA GHARAMA ZA FEDHA ZINAZOTAKIWA KULIPIA NISHATI MBADALA KWA KIASI KIKUBWA SANA

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *