KILA NYUMBA INA UPEKEE WAKE, KILA MTU ANA LADHA YAKE KIPEKEE.

Kwa mtazamo wa ujumla watu hufikiri kwamba anaweza kupenda na kuridhishwa na nyumba ambayo tayari imeshachorwa au kufikiri kwamba kazi ambayo umeshaifanya unaweza kumpa tu mtu mwingine akaenda kuijenga kama ilivyo, lakini jambo la ajabu ni kwamba katika asilimia 100% ya wateja wanaohitaji nyumba, labda ni asilimia 1% tu ndio wanaoweza kuchukua ramani kama ilivyo na kuridhika nayo, asilimia 99% zilizobaki utakuta wanahitaji mabadiliko kadhaa ili kuweza kukubaliana na nyumba husika. Hili ni jambo ambalo hata mimi binafsi limekuwa likinishangaza lakini mara zote huwa hivyo tofauti na wengi wanavyoweza kufikiri.

LADHA TOFAUTI ZA WATU NDIO HULETA UPEKEE UNAOUONA

Unapokutana na mteja anahitaji kufanyiwa kazi yake utakuta anakwambia umuonyeshe kazi zako nyingine ili achague kwamba amependa ipi, lakini ni mara chache kuridhishwa na yoyote kwa asilimia 100% hata kwa mtazamo wa nje peke yake, japo yeye mwenyewe atakubali kwamba kweli hizo ni kazi zilizofanyika kwa viwango vya juu sana. Mkiingia ndani ya jengo kuangalia mpangilio wa vyumba na nafasi nyingine ndani ya nyuma ndio kabisa hujikuta akifanya machaguo tofauti na namna nyumba hiyo imepangiliwa. Nilichojifunza ni kwamba kila mtu ana ladha yake ya kipekee ambayo haifanani na ya mtu mwingine yeyote kwa asilimia 100% japo hata yeye mwenyewe anaweza asijue hilo, na hilo linapelekea kila nyumba kuwa na upekee wake ambao sio rahisi kumridhisha mtu mwingine kwa asilimia 100% tofauti na mhusika aliyeichagua. Sasa unapoongezea na vitu vingine kama hali ya uchumi, mazingira husika na hali ya hewa iliyopo, kanuni za taaluma husika na vigezo na masharti vilivyowekwa na mamlaka husika ndio unakuta kwamba kila nyumba huja na upekee wake wa tofauti kabisa.

MAZINGIRA YA NJE PIA HUCHANGIA KULAZIMISHA KULETA LADHA YA TOFAUTI

Hivyo unapoamua kuanza kufanya nyumba yako ni vyema kujua hasa vitu unavyovipenda kisha kujifunza zaidi na kuangalia kazi mbalimbali zilizofanyika tayari na kujua nini unapenda na nini hupendi, kisha baada ya hapo kuonana na msanifu na kumwambia vyote kisha utengenezewa nyumba inayoendana na mahitaji, matakwa na matamanio yako ambayo ni ya kipekee kabisa kuliko kujaribu kuhangaika kutafuta ambayo imeshafanyika tayari. Sipingi suala la kujaribu kutaka kuona kazi zilizofanywa na mtaalamu husika, naunga mkono kabisa hilo na nasisitiza kabisa kwamba ni muhimu kufanya hivyo ili angalau ujue uwezo wa mtaalamu husika lakini naona huhitaji kukazana kulazimisha kazi ambazo tayari zimeshafanyika ziendane na unavyotaka wewe, hilo ni jambo ambalo sio rahisi kutokea badala yake unachotakiwa ni kujua hasa nini unataka na nini hutaki kutoka kwenye kazi zilizoshafanyika kisha wewe kufanya ya kwako ya kipekee kabisa ambayo nayo wengine watakuja kuiangalia kuona ni nini wamependa hapo na nini hawajapenda kuweza kuja na ladha zao nyingine za kipekee.

ANGALIA KAZI NYIGINE KWA LENGO LA KUJIFUNZA NINI UNAPENDA NA NINI HUENDI

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *