GHARAMA ZA UJENZI ZINABADILIKA KUTEGEMEA NA MACHAGUO UNAYOFANYA.

Mara nyingi watu hupenda kuulizia gharama za ujenzi wa jengo au nyumba fulani aidha ya chini au ya ghorofa kutaka kujua bei ili ajue kama yuko kwenye nafasi kubwa kiasi gani kuweza kuijenga. Ni sahihi kabisa na ni jambo muhimu kuweza kufahamu hili ili kujua ni kiasi gani unaweza kumudu na kwa muda gani utaweza kukamilisha mradi husika kutokana na bei yake pamoja na nafasi yako kifedha.

MWISHO WA UJENZI UTAKUTA GHARAMA ZIMEONGEZEKA SANA TOFAUTI NA MAKADIRIO YA MWANZONI

Lakini kuna kitu kimoja cha muhimu hapa mtu anatakiwa kufahamu baada ya kuwa amefahamu wastani wa gharama ya mradi husika kwamba gharama mara zote huongezeka sana kutegemea na machaguo utakayofanya kwani makadirio ya gharama hiyo unayopewa yanatokana na machaguo fulani ambayo yamefikiriwa kwamba ndiyo utakayoyafanya kitu ambacho kinaweza kubadilika kwa wewe kubadili mawazo baada ya kugundua faida au changamoto za chaguo husika hapo baadaye.

CHANGAMOTO NA UFAHAMU ZAIDI JUU YA MACHAGUO YA MWANZO ZITAKUFANYA UBADILISHE SANA MACHAGUO YAKO KATIKA YA MRADI

Kwa mfano gharama husika inaweza kuwa imekadiriwa kwamba utatumia bati ya geji 30 kuezeka nyumba yako, lakini baadaye ukagundua kwamba bati ya geji 30 sio nzito sana na pengine ungetaka bati nzito na imara zaidi ambapo ukaamua kuchagua beti ya geji 26 ambayo gharama yake ni kubwa zaidi ya geji 30 hivyo mwisho wa siku utakuta gharama ya jumla tayari inaongezeka. Hilo lina kwenda kwenye kila kitu kwa sababu katika ujenzi kila kifaa unachotumia kina ngazi mbalimbali za ubora na bei ambapo utakuta kwa nyumba hiyo hiyo mtu anaweza kujenga kwa mara mbili ya bei ambayo mtu mwingine amejenga kwa sababu ya machaguo ya vifaa na hata huduma za kiufundi za wataalamu wanaoijenga kutokana na ubora wao.

UBORA WA VIFAA NA HUDUMA ZA KIUFUNDI ZINATOFAUTIANA BEI KWA KIASI KIKUBWA

Ni muhimu kujua mapema hasa unachotaka ili uweze kufanya maamuzi sahihi ukiwa unaelewa kwa usahihi utofauti gharama na ubora.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *