KUPANGA GHARAMA ZA UJENZI.

Gharama za ujenzi ni kati ya vipengele muhimu sana kila mara mtu anapofikiria kuhusu ujenzi wa mradi wowote wa ujenzi kwa sababu, gharama za ujenzi ndizo zinazoamua endapo mradi husika utajengwa na kwa kiwango au ukubwa gani mradi huo utajengwa. Na ukweli ni kwamba gharama za ujenzi siku zote hutofautiana kati ya mradi mmoja na mwingine kwa sababu tofauti tofauti hata kama ni miradi inayofanana kwa kila kitu. Karibu mara zote gharama za ujenzi huwa kubwa zaidi ya bajeti iliyowekwa kwa karibu miradi yote, na kama hakukuwa na umakini mkubwa wakati wa makadirio mwanzoni basi bajeti huweza kuwa kubwa sana kuliko ilivyokuwa inategemewa. Kushindwa kupangilia gharama za ujenzi kumesababisha baadhi ya miradi ya ujenzi kuishia njiani kwa sababu bajeti iliyotegemewa kumaliza mradi imeishia njiani na hakuna chanzo kingine cha mapato cha kumalizia mradi husika.

KUPANGA GHARAMA ZA UJENZI KUNAEPUSHA MRADI WA UJENZI KUISHIA NJIANI

Sasa kuna falsafa inayojulikana kama “Kupanga gharama”, au “Cost planning” ambapo wataalamu wa masuala ya ujenzi wanakutana pamoja na mteja kujadili namna kazi itakavyofanyika ndani ya bajeti iliyopo ambapo msanifu majengo anakuwa ametengeneza michoro ya mwanzoni ya mapendekezo ambayo yatajadiliwa pamoja na mtaalamu mkadiriaji majenzi kuangalia vitu vya kuongeza na kupunguza ili mradi husika ulingana na bajeti ya iliyopo. Kwa kufanya hivi mradi husika kuanzia kwenye kuandaa michoro pamoja na vitu vingine vyote vitakavyojumuishwa vinakuwa vinaamuliwa na bajeti iliyopo. Mkadiriaji majenzi atakuwa anafanya kazi kwa karibu na msanifu majengo kuhakikisha vitu muhimu vinakuwepo na visivyokuwa muhimu vinaondolewa na kupunguza baadhi ya vitu kadiri ya matakwa ya mteja na umuhimu wa vitu hivyo kitaalamu mpaka kuhakikisha jengo linajengwa kwa usahihi na kwa kadiri ya bajeti ya mradi huo inavyoruhusu.

KUPANGA GHARAMA ZA UJENZI KUNASAIDIA KUPUNGUZA VITU VISIVYO VYA LAZIMA VINAVYOONGEZA GHARAMA KATIKA JENGO

Kwa kufanya hivi mradi wa ujenzi unakuwa na uhakika wa kujengwa mpaka kumalizika ndani ya bajeti iliyopo huku ukitimiza mahitaji yote muhimu tayari kwa matumizi. Hii ni moja kati ya mbinu muhimu ya kupunguza uwezekano wa miradi kuishia njiani, hasa miradi mikubwa.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *