RANGI ZA JENGO.

Mpangilio wa rangi katika jengo ni kati ya vipengele vya ujenzi vyenye utata na vinavyoleta wakati mgumu sana katika kuchagua mpangilio sahihi. Japo kuna watu wataalamu na wabobezi kwenye masuala ya mpangilio wa rangi lakini suala la rangi mara nyingi kila mtu huwa na ladha yake tofauti anayoipenda au kuvutiwa nayo na mara nyingi huwa hana sababu ya kupenda hiyo bali ni suala la hisia zaidi kwamba rangi fulani inampendeza. Jambo hili kwa kiasi limekuwa changamoto kidogo katika kufanya maamuzi juu ya upi mpangilio sahihi wa rangi katika jengo kwa sababu wakati mtu anayesimamia upakaji rangi anafikiria kuhusu mpangilio wa rangi fulani na fulani au mchanganyiko na mpangilio zaidi mteja mwenye jengo anavutiwa na aina nyingine za rangi ambazo mtaalamu mwenyewe anafikiri zinapunguza ubora wa kimuonekano.

MPANGILIO SAHIHI WA RANGI KWENYE UJENZI NI SUALA LA MTAZAMO BINAFSI ZAIDI KULIKO KANUNI FULANI INAYOKUBALIKA NA WATU WOTE.

Hivyo basi suala la rangi ni vyema sana endapo litatuliwa mapema kabisa kuanzia wakati wa kuandaa michoro ambapo mjadala wake unatakiwa kufanyika kwa kina na michoro ipangiliwe kwa usahihi sana sawa na vipaumbele vilivyofikiwa katika makubaliano ya mwanzoni juu ya rangi. Lakini endapo kazi imeshafanyika na hakukuwa na makubaliano yoyote mwanzoni au jengo limejengwa bila picha ya mwonekano wa nje basi ni vyema kutafuta mwonekano wa picha mbalimbali za majengo mengine na kuangalia mipangilio mbalimbali na kuzijadili na kuamua ni mpangilio wa namna gani unaenda kutumika hapo. Mpangilio sahihi ukishaamuliwa utahitajika kukubaliana pia namna unaenda kuingizwa katika jengo husika kwa sababu picha ya jengo ambalo mpangilio huu umetokea sio rahisi ukute linafanana na jengo linalojengwa kwa kiasi kikubwa.

PICHA YA JENGO HUSAIDIA KATIKA MAAMUZI SAHIHI YA MPANGILIO WA RANGI KATIKA JENGO NA KUTOA MWONGOZO KWA USAHIHI KATIKA KUJENGA

Ni muhimu sana na itakuwa na maana zaidi endapo suala hili litatatuliwa mapema kabisa mwanzoni kwa kupata mpangilio sahihi ulioridhiwa na pande zote au kama muda na bajeti inaruhusu basi kazi hiyo ya kutengeneza mwonekano wa picha za jengo husika kuonyesha mpangilio wa rangi inaweza kufanyika kwanza na baada ya picha kukamilika ndipo ujenzi uendelea katika upakaji wa rangi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *