UBORA WA VIFAA VYA UJENZI NA UFUNDI NDIO UBORA WA JENGO LENYEWE.

Wote tunakubaliana kwamba ubora wa mradi wa ujenzi upo kwenye ubora wa usimamizi kwa ujumla, ambapo ndipo tunakuja kukuta kwamba usimamizi sahihi ni ule unaohakikisha ubora umezingatiwa kwa kuzingatia orodha ya mambo muhimu yanayojumuisha ubora wa vifaa na ubora wa ufundi wa jengo. Unapokuwa na vifaa vya ujenzi vyenye ubora bila kuhakikisha kwamba ufundi nao ni wa viwango vya juu unakuwa umefaulu nusu ya mtihani na nusu nyingine umefeli kwa sababu utatumia gharama kubwa kwenye vifaa kujenga jengo lenye changamoto nyingi za kiufundi na hata kuja kuingia gharama kubwa zaidi kufanya marekebisho baadaye. Hali kadhalika ukitumia ufundi wa viwango vya juu lakini huku ukitumia vifaa vya ujenzi vilivyokosa ubora utaishia kupata matokeo mazuri lakini yasiyodumu kwa muda mrefu vya kutosha na hivyo bado utakuwa upande wa hasara.

MCHANGANYIKO WA VIFAA BORA NA UFUNDI BORA HULETA MATOKEO BORA SANA

Ujenzi makini unazingatia sana ubora kwenye kila eneo kwa sababu ubora wa maeneo yote kwa pamoja ndio unaoamua ubora wa jengo kwa ujumla. Watu wengi wana udhaifu mkubwa kwenye eneo la ubora wa ufundi, kwamba wanaingia gharama kubwa kununua vifaa vya ujenzi vya gharama kubwa lakini wanashindwa kuweka kipaumbele kwenye ufundi wa viwango vya juu na changamoto ni kwamba ufundi usiokuwa wa viwango sahihi huwezi kuuona mwanzoni na pengine unaweza usiouone kabisa hata mpaka jengo linakamilika ikiwa wewe sio mtaalamu wa masuala ya ujenzi hivyo unaweza kuona uko salama lakini matokea ya udhaifu wa kiufundi unaweza kuja kuyaona baadaye baada ya jengo kuwa limeanza kutumika. Jambo la kwanza na la msingi sana ni kupata kwanza usimamizi sahihi ambao una uzoefu wa viwango cha juu vya ubora, hii itasaidia kwanza kujiepusha na vitu visivyo na ubora tangu mwanzoni kwa sababu uko na mtaalamu ambaye hawezi kukubali viwango vya chini vya ubora kwa namna yoyote ile na hapo mtaanza kupanga namna sahihi ya ujenzi inayozingatia ubora unaotarajiwa.

MATOKEO YASIYOFAA UTAYAONA KWA KUCHELEWA UKIWA TAYARI UMEFANYA KOSA NA KUPATA HASARA

Kwa mtu usiye na uzoefu ubora wa jengo ni kitu ambacho huwezi kukiona kiurahisi hasa mwanzoni hivyo ni vyema kuweka umakini mkubwa katika namna ya kutekeleza mradi wako wa ujenzi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *