THAMANI YA HUDUMA YA KITAALAMU IKO KWENYE MUDA, UTAALAMU NA UZOEFU.

Katika vitu ambavyo nchi nyingi ambazo ziko nyuma kimaendeleo zimekuwa hazioni thamani kubwa kwake ni suala la muda. Kimsingi muda ni kitu cha thamani kubwa sana kuliko hata pesa kwa sababu pesa zilizopotea zinaweza kutafutwa zikapatikana lakini muda uliopotea hauwezi kutafutwa ukapatikana. Kila kitu cha thamani unachoweza kuzalisha unatumia muda kukizalisha na ukikosa muda maana yake kitu hicho huwezi kukizalisha na huwez kupata hiyo thamani kwa maana ya kitu hicho au fedha ambazo zinawakilisha thamani ya kitu cha kiwango hicho. Lakini muda pia ndio maisha yako na uhai wako na kadiri unavyozidi kupotea ndivyo unavyoendelea kupoteza kitu cha thamani sana kwako ambacho ni sehemu ya maisha yako au sehemu ya uhai wako. Watu wengi wamekuwa hawathamini muda kwa sababu hawaoni thamani hii kubwa sana ya muda na hivyo kuchukulia muda kama sio kitu cha thamani sana pale wanapohesabu thamani ya kitu wanacholipia.

MUDA UNAOTUMIKA KUFANYA KITU KIMOJA NI THAMANI YA MUDA ULIOPOTEZWA BADALA YA KUFANYA KITU KINGINE(OPPORTUNIST COST)

Sasa inapokuja kwenye suala la huduma ya kitaalamu watu wakiangalia thamani ya huduma ambayo mtu anaitoa wanaangalia ufanyaji wa kazi pekee na changamoto zake bila kufikiria kabisa kuhusu muda ambao mtu anatumia katika kufanya kazi ile, utaalamu ambao mtu anauweka pale ambao alitumia muda mwingi sana kuutengeneza na kuugharamia pia pamoja na uzoefu wa miaka mingi ambao ameweka katika kujijenga mpaka kufikia ubobezi mkubwa alionao kiasi cha kuweza kutoa huduma yenye ubora mkubwa kiasi hicho. Kwenye suala la muda mtu anapoacha kufanya vitu vingine vyote na kupeleka muda huo kwenye kazi hiyo maana yake ameacha starehe zote, muda wa kukaa na familia, fursa za kuwa karibu na watu wake muhimu, kutumia nguvu za mwili na akili ambazo zina ukomo, kusoma vitabu kuongeza maarifa, kazi zake zote za nyumbani, kukuza mtandao wake wote wa kazi, kuacha kufanya kazi nyingine za kujiingizia kipato ili muda huo auweke kwenye kazi hiyo hapa maana yake ameacha vitu vyote muhimu ili ahangaike na kazi hiyo ambayo anaifanya kwa sababu anahitaji kuongeza kipato cha fedha anachohitaji kwa ajili ya kuboresha hayo mengine. Suala la pili ni utaalamu, huo utaalamu ambao mtu anauweka kwenye kazi husika ili iwe bora na ya viwango sahihi ametumia muda mwingi sana kuutafuta kwa mfano miaka aliyokaa chuoni akisoma pamoja na gharama kubwa aliyolipia kuusoma, pamoja na muda wa miaka aliyotumia kusoma katika kuutafuta huo utaalamu alikuwa ana uwezo wa kutumia muda huo vinginevyo. Suala lingine ni uzoefu ambao mtaalamu husika ameukusanya kwa kufanya kazi nyingi za namna hiyo kwa miaka mingi pamoja na kujifunza kutokana na makosa mengi ya nyuma ambapo pia alitumia muda mwingi badala ya kuweka kwenye mambo mengine ambao unasaidia katika kuboresha huduma ya kazi husika nayokupatia. Mjumuisho wote huo hasa huo wa suala la muda ndio unaoipa huduma husika thamani kubwa ambayo watu wengi huwa hawaioni. Ni rahisi mtu kusema hii kazi ni rahisi tu mbona hata mimi nikiwa na muda ninaweza kuifanya mwenyewe au kwani unatumia gharama gani kunifanyia kazi hii, lakini kazi hiyo bila utaalamu itakuwa mbovu sana na hata hasara ambayo mtu anaweza kuingia kwa kufanya kazi hiyo mbovu ni kubwa kuliko gharama ya utaalamu anayoikwepa.

UZOEFU WA MIAKA MINGI ULIOLIMBIKIZWA KWENYE KUJENGA UTAALAMU UNAKUWA UMETUMIA GHARAMA ZAIDI YA MUDA NA FEDHA NA KUONGEZEKA SANA THAMANI

Sheria ya asili mara nyingi haifeli kwenye kuamua thamani ya vitu, thamani ya huduma haitofautiani na thamani ya bidhaa bora, kama jinsi ilivyo mtu anahitaji fedha ya kutosha kununua gari ya thamani zaidi ndivyo mtu anahitaji fedha ya kutosha kugharamia huduma yenye thamani kubwa, vinginevyo atapata thamani isiyo ya viwango sahihi ambayo mara nyingi itamgharimu.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *