STAILI ZA UJENZI KATIKA NYAKATI ZA NIOLITIKI TANGU MIAKA 12,000 ILIYOPITA

Historia ya ujenzi na staili za kujenga zinaenda miaka mingi nyuma mpaka katika nyakati za kipindi cha niolitiki miaka zaidi ya 12,000 iliyopita wakati yalipoanza mapinduzi ya kilimo na binadamu kuanza kuwa na makazi ya kudumu na kuishi katika jamii za pamoja kwa idadi kubwa huku imani mbalimbali za kidini zikianza kusambaa na kuwaunganisha watu kwa wingi na kwa eneo kubwa. Katika wakati huu kulikuwa na mchanganyiko kidogo wa staili ya makazi ya miaka ya nyuma ambayo mengi yalikuwa ni kama mapango yaliyotengenezwa vizuri kwa staili ya makazi na makazi ya kujengwa kumudu mahitaji yote muhimu ya nyakati hizi za mapinduzi ya kilimo. Katika ujenzi wa nyakati hizi za niolitiki watu walianza kutumia udongo wa mfinyanzi kujenga kuta lakini japo hakukuwa na staili za kibunifu au maendeleo ya sana lakini walianza kuwa na urembo wa kuchora kwenye kuta. Katika kusini na kusini magharibi mwa Asia au mashariki mwa bahari ya mediterania tamaduni za ujenzi za kiniolitiki zilianza tangu miaka 12,000 iliyopita hasa katika eneo lililojulikana zamana kama Levante ambalo leo hii linajumuisha nchi za Syria, Lebanon, Jordan, Israel, Palestina na Uturuki ya kusini.

MJI WA ZAMANI ZAIDI WA GOBEKLI TEPE ULIOJENGWA MIAKA 12,000 ILIYOPITA HUKO UTURUKI

Miji iliyoendelea katika nyakati hizi za niolitiki zenye staili za ujenzi za teknolojia ya nyakati hizi ni pamoja na Gobekli Tepe wa eneo lilijulikana zaidi zamani kama Anatolia ambalo ni eneo la Uturuki ya leo miaka 11,000 iliyopita, mji wa Yeriko ulioendelea miaka 10,350 iliyopita, Nevali Cori Uturuki ya leo miaka 10,000. Maeneo mengi pia kama Mesopotamia ya zamani, Asia ya kati, Syria n.k. yaliendeleza harakati nyingi za ujenzi kwa kujenga miji ya zamani sana na nyumba nyingi za vijiji kwa kutumia matofali ya udongo/tope. Katika majengo haya waliweka zaidi urembo wa michoro ya watu na wanyama pia kama ubunifu wa kisanaa wa kupendezesha maeneo yao. Katika kipindi hiki hiki cha niolitiki huko Malta katika eneo la kati la bahari ya mediterania waliweza kujenga mahekalu makubwa waliyoyatumia kama majumba ya kuabudiwa yakiwa ni mahekalu ya mwanzo kabisa yaliyotumiwa na binadamu kwa ajili ya ibada miaka 7,000 iliyopita. Kipindi hiki pia cha niolitiki kilichoanza katika nyakati za mapinduzi ya kilimo tangu miaka 12,000 iliyopita mpaka miaka 4,000 iliyopita maendeleo mengine ya ujenzi wa aina ya tofauti ilikuwa ni ujenzi wa makaburi ambapo mpaka leo bado kuna makaburi mengi yaliyojengwa huko Ulaya ambayo yalijengwa katika teknolojia na staili za ujenzi za kipindi cha niolitiki.

MOJA KATI YA NGUZO ZA UKUTA ZENYE UREMBO KATIKA MJI WA ZAMANI WA GOBEKLI TEPE HUKO UTURUKI YA ZAMANI MIAKA 12,000 ILIYOPITA

Kipindi cha niolitiki ni kipindi cha baada ya zama za mawe za mwisho ambapo kulianza kutokea mapinduzi makubwa ya maendeleo ya ujenzi na staili mbalimbali za ujenzi za mwanzoni kabisa ambazo zilijengwa kwa tekonolojia ya zama iliyojumuisha makazi ya watu, vijiji na miji ya zamani.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *