KUBADILI MATUMIZI YA KIWANJA

Changamoto kubwa sana ambayo watu wamekuwa wakikutana nayo mara kwa mara wanapokuwa wanashughulika na kibali cha ujenzi ni suala la matumizi ya kiwanja. Eneo la matumizi ya kiwanja limekuwa ndio eneo linaloongoza kwa kukwamisha miradi mingi zaidi ya ujenzi.

Changamoto iliyopo ni kwamba eneo la matumizi ya kiwanja lina vipengele vingi sana ambavyo vimegawanyika katika vipengele vingine vidogo vidogo vingi zaidi.

Suala hili la matumizi ya kiwanja kuwa katika vipengele vilivyogawanyika katika vipengele vingine vidogo zaidi limepelekea miradi mingi ya ujenzi kukwama kwa sababu mtu hufikiri kwamba mradi wake unaendana na matumizi husika lakini anapofika kupitisha michoro ya ramani za ujenzi anakuta kipengele kidogo hakiendani na matumizi husika.

BANGO LA MATUMIZI YA KIWANJA YANAPASWA KUKAA KATIKA ENEO LA UJENZI KWA ANGALAU MWEZI MMOJA

Hivyo hapo mtu anajikuta analazimika aidha kubadili matumizi ya kiwanja yaendane na mradi wake wa ujenzi au kubadili mradi wa ujenzi uendane na matumizi ya kiwanja. Kwa sababu mtu unakuta anachohitaji ni mradi wake wa ujenzi kujengwa hivyo kubadili matumizi ya kiwanja ndio mbadala ambao mara nyingi hufuatwa na wengi huku wachache wakiamua kubadili mradi uendane na kiwanja.

Kubadili matumizi ya kiwanja kiendana na mradi wa ujenzi huwa ni mchakato mrefu zaidi ukilinganisha na kubadili mradi wa ujenzi uendane na matumizi ya kiwanja na mara nyingi uko nje ya maamuzi yako japo wengi hufanikisha baada ya kupitia katika hatua na vitengo kadhaa katika wizara ya ardhi.

NAKALA YA BANGO LA KUSUDIO LA KUBADILI MATUMIZI YA KIWANJA LINATAKIWA KUAMBATANISHWA KWENYE NYARAKA ZA KWENDA WIZARA

Kubadili matumizi kiwanja yaendane na mradi wa ujenzi kwanza unatakiwa uwe na michoro yote ya ramani za ujenzi ambao unalenga kuufanya baada ya kubadili matumizi, iliyopigwa mihuri pamoja na hati ya kiwanja. Hapa utaanza kwanza kwa kutengeneza bango kubwa la kutangaza rasmi kubadili matumizi ya kiwanja husika ambalo litakaa katika eneo la kiwanja chako kwa muda wa mwezi mmoja.

Baada ya mwezi mmoja endapo hakutakuwa na pingamizi lolote la tangazo hilo la kubadili matumizi basi utawasilisha nyaraka zako katika wizara ya ardhi kuanzia nakala ya bango hilo, michoro ya ramani za jengo unalotaka kujenga, barua ya kuomba kubadili matumizi, nakala ya risiti za malipo ya kodi ya ardhi, nakala ya hati ya kiwanja na ramani yam choro wa mipango miji.

WIZARA YA ARDHI ITAKUPA GHARAMA ZA KULIPIA MADILIKO YA MATUMIZI NA KUKUPATIA HATI YA MABADILIKO ITAKAYOPELEKWA KWENYE HALMASHAURI HUSIKA

Baada ya kuwasilisha nyaraka hizi utapewa gharama ya kulipia mabadiliko hayo ya matumizi na kisha mchakato wa kubadili matumizi hayo utafanyika wizara kisha utapatiwa hati za mabadiliko ya matumizi ambazo zitapelekwa pia kwenye halmashauri husika kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kupatiwa kibali cha ujenzi.

Hivyo ni vyema kufahamu mapema endapo mradi unaojenga utalazimika kuhusisha mabadiliko ya matumizi ya jengo na kisha kuanza mchakato huo mapema ili kuokoa muda.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *