USIPOTEZE MUDA KUFIKIRIA KAZI YOTE, UJENZI NI SAFARI NDEFU NA INA VITU VINGI.

Watu wengi wamekuwa wanasita sana kwenye kuchukua hatua yoyote kwa kufikiria sana jinsi ya kumaliza mradi mzima wa ujenzi tangu mwanzoni, kitu kinachopelekea watu kusita kuchukua hatua na wengine kuahirisha hata kujenga kwa wakati huo akisubiri siku ambayo atakuwa tayari amefanikisha mambo mengi sana kuhusu mradi huo na miaka mingi kupita kabla hajafanya hivyo.

Kuna usemi mmoja wa kiswahili unasema ukitaka kumla tembo unaanza kwa kumkata vipande vidogo vidogo. Ikimaanisha huwezi kumla tembo mzima kwa pamoja na huwezi kumla tembo kwa siku moja, lakini hiyo haimaanishi kwamba huwezi kumla tembo mzima ukammaliza. Licha ya kwamba tembo ni mnyama mkubwa sana lakini unaweza kumla na ukammaliza lakini haitakuwa siku moja wala hautammeza kwa pamoja, anahitaji mikakati mikali kuanzia kumkamata.

Huo ni mfano muhimu sana katika miradi mikubwa hususani ujenzi. Kwanza kabisa ujenzi licha ya gharama zenyewe za ramani na ujenzi kuna mambo mengine mengi muhimu yasiyohitaji pesa unayopaswa kuhangaika nayo ikiwemo uelewa wa mambo mengi ya kitaaluma na kisheria kuhakikisha kwamba mradi wako uko katika utaratibu sahihi ili usijikuta unaingia kwenye hasara na majuto.

Lakini kitu cha msingi sana cha kufahamu ni kwamba bajeti ambayo unaifikiria kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo kuna uwezekano mkubwa haitamaliza kazi hiyo hata kama umeifanya kwa ushirikiano na wataalamu wa ukadiriaji majenzi. Hivyo chochote kinachokukwamisha kuanza mradi wako wa ujenzi unatakiwa ukipuuze na kuanza mara moja kwa kuanzia popote unapoweza kuanzia.

Kama una nia kweli ya kujenga anza, na ukishaanza na kuelewa mambo mengi zaidi utaendelea kupanga mambo mengine zaidi ya mbeleni ambapo utakutana na mengi usiyoyategemea pia. Kwa kupitia kuelewa mambo mengine zaidi utafanya pia maamuzi mengi tofauti yanayoendana na kile unacholenga ambapo mara nyingi utajikuta hata unabadilika pia kutoka kwenye mtazamo uliokuwa nao mwanzoni.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *