USITEKWE NA HOFU YA GHARAMA UKASAHAU MAMBO MUHIMU KWENYE JENGO.

Sisi binadamu ni viumbe wa hisia na ndio maana hata maamuzi yetu mengi huongozwa na hisia zaidi kuliko mantiki, na moja kati ya vitu ambavyo huteka sana hisia zetu ni vitu vinavyopatikana kwa uhaba na vyenye thamani kubwa. Fedha ni kati ya rasilimali zinazopatikana kwa uhaba na thamani yake ni kubwa ni hiyo ndio sababu huwa vinateka sana hisia zetu pale tunapofikiria kuhusu matumizi yake na moja kwa moja hisia hutupeleka kwenye kuhakikisha tunailinda rasilimali hii adimu na yenye thamani.

Hii ndio sababu watu wengi sana wanapofikiria kuhusu jambo lolote linalohusisha fedha huwa moja kwa moja hisia za uhaba huwajia na kufikiria namna watahakikisha inatumika kwa uchache inavyowezekana bila hata kufikiria kama kiasi hicho cha fedha ndio kinastahili au la au kama kiasi hicho cha fedha kinanunua bidhaa au huduma yenye ubora au la, bali mara zote mtu huwaza kuhakikisha inatumika kwa uchache sana ili iweze kubaki kwa ajili ya matumizi zaidi.

Huu naweza kusema ni udhaifu tulionao kwa kiasi kwa sababu, licha ya kwamba ni muhimu sana kuwa makini sana katika matumizi ili watu wasikuibia au kukutoza zaidi ya vile inavyostahili lakini kwa wengi wetu hisia hizi huwa kali na kwenda mbali zaidi kiasi cha kutupiga upofu kwenye maeneo mengine muhimu ya kutazama katika mchakato huo wa manunuzi na badala yake hisia, nguvu na akili zote kubaki kwenye kupunguza gharama peke yake bila kujali madhara yake.

Udhaifu huu tunakutana nao pia sana katika ujenzi ambapo mtu kwa kuwa unakuwa uko upande wa pili wa mtazamo wa mtu basi unaona kwa uwazi jinsi mtu anaweza kuweka hisia, nguvu na akili kwenye kuhangaika na gharama pekee na hilo kupelekea kusahau au kupuuza maeneo mengine ambayo yana umuhimu mkubwa na hivyo kujikuta kwenye hasara kubwa zaidi ya gharama aliyokuwa anajaribu kukwepa.

Kwa mfano unakuta mtu ametekwa kwenye kutazama gharama peke yake na hivyo katika hatua ya michoro anafanya kazi na mtu asiye na viwango bora na kumfanyia kazi duni ambayo inatumia gharama kubwa kwenye malighafi lakini yenye mapungufu makubwa kitaaluma, au unakuta mtu ananunua malighafi za gharama kubwa lakini hataki kuweka usimamizi bora hivyo anajikuta amenunua malighafi za bei ghali kujenga nyumba ya viwango duni ambapo ilitakiwa aweke msisitizo na kwenye usimamizi ili maighali za bei ghali alizonunua zifanyike kwa usahihi unalingana na hadhi yake.

Hivyo ni muhimu sana pale mtu unaposhughulika na mradi wako wa ujenzi kuhakikisha kwamba unatafuta uwiano mzuri wa kutafakari kazi hiyo ya ujenzi ili uweze kuhakikisha hutawaliwi na hofu ya gharama peke yake bali unajaribu kuangalia na ubora wa matokeo kwa kufikiria ni wapi muhimu pa kuongeza mkazo badala ya kukimbilia urahisi wa gharama ambao unaweza kukufikisha kwenye majuto.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *