KUJUA GHARAMA HALISI ZA UJENZI WA NYUMBA YAKO.

Imekuwa kawaida mtu kukupigia simu kutaka umwambie gharama ambazo mradi wake wa ujenzi utagharimu kwa ujumla kwa kukwambia mahitaji yake na hadhi ya kiwanja chake. Suala hili limekuwa lina utata kidogo kwa sababu kwanza nimekuwa nikitaka kwanza kujibiwa maswali kadhaa ambayo mara nyingi mhusika anakuwa aidha hana majibu ya moja kwa moja au hajafanya maamuzi bado na hapo ndipo inakuwa changamoto sana kwani najikuta nahitajika kutoa majibu ambayo yanakosa uhalisia.

Ukweli ni kwamba ni vigumu kujua gharama halisi za ujenzi wa mradi wa jengo kama haujafanyika mjadala wa kina wa kuamua juu ya namna kazi yote itafanyika na hasa aina ya malighafi zitakazotumika kwani ni eneo ambalo linaleta utofauti mkubwa sana kwenye suala la gharama kwa sababu ya utofauti mkubwa uliopo baina ya kile watu wanapenda na kuthamini na gharama zake.

Changamoto huwa kubwa zaidi pale ambapo mtu anakuficha kile haswa anachotaka kufanya kwa sababu pengine ya kuhofia usije kumwona ana uwezo mkubwa tofauti na vile yeye anataka umfahamu ili usaidie katika kupunguza gharama za ujezi wa mradi wake, suala ambalo hata hivyo huweza kuathiri vibaya matokeo ya mwisho na kusingekuwa na madhara sana kama ukweli ungejulikana.

Kufahamu gharama halisi za ujenzi kunahitaji mtu kufahamu kwa uhakika ni vitu gani anatamani kutumia ndani ya nyumba yake kwa maana ya aina ya malighafi ambazo huwa ziko katika viwango tofauti vya ubora na aina tofauti ya mwonekano na ubunifu na bei zake pia hutofautiana sana. Lakini katika kutaka kufahamu bei ya ujenzi mara nyingi mteja anakuwa hajaweka wazi juu ya machaguo yake haya lakini wakati wa ujenzi ukifika anajikuta ananunua malighafi ya gharama tofauti na zile zilizopendekezwa.

Kwenye suala la ufundi pia utofauti huu hujitokeza ambapo baada ya mteja kufahamu utofauti wa ubora uliopo baina ya mafundi na hata wakati mwingine baada ya uwezo wa fundi fulani kuonekana basi huamua kufanya machaguo tofauti ambayo huleta utofauti wa gharama pia na kupelekea bei iliyokuwa imekadiriwa mwanzoni kuwa tofauti na inayokuja kutokea katika uhalisia.

Hivyo ni muhimu sana katika kujadili gharama za ujenzi kabla ya ujenzi kuanza kuwe na mjadala mpana wa vitu vingi na hasa kwenye upande wa malighafi kujadili mibadala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uimara wake, mapungufu yake na utofauti wake wa gharama kisha kuwe na uhuru wa kufanya maamuzi na kutokea hapo ndipo gharama za ujenzi zikadiriwe. Kwa utaratibu huo gharama zilizokadiriwa zitakuwa kwenye uhalisia mkubwa zaidi na mteja atakuwa na taarifa sahihi zaidi ambazo sio rahisi kuja kubadilika sana baadaye.

Karibu sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *