MSINGI WA JENGO UNAPOKOSEWA.

Kwa kawaida siku zote ujenzi huwa unaanza na kitu kinachoitwa “setting out”, yaani kuli-set jengo katika eneo sahihi ambapo litakaa. Hatua hii huwa ni muhimu sana kwani ndio inayoamua uelekeo wa jengo na namna linahusiana na kiwanja linapojengwa lakini muhimu zaidi ni hatua hii inapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa ili kupata usahihi wa mraba wa jengo ambao ndio utaamua vitu vingi sana katika ujenzo huo.

Msingi wa jengo ndio unaotoa uelekeo wa jengo lenyewe hivyo usahihi wa ule mraba wa jengo maarufu kama “square” ndio unaokuja kuamrisha mpangilio wa vipengele vyote vinavyojengwa na hivyo mraba huo unapokosekana vipengele vingi vinavyokuja kujengwa vinakosa mpangilio sahihi. Hii ni kwa sababu karibu vifaa karibu vyote vya ujenzi vinavyotengenezwa huwa vinazingatia kanuni ya mraba huu ili vinavyojengwa visipoteze ule uzuri wa kimpangilio.

New Home Foundation Construction

Vitu kama vigae vya sakafuni, vifaa vya mabafuni, makarai ya kuogea, fremu za milango na madirisha, samani zote za ndani ya nyumba mpangilio wa mbao au chuma za mapaa zote hufuata kanuni hii ya usahihi wa mraba wa jengo hivyo jengo linapokuwa limekosewa katika kusetiwa kwenye msingi basi makosa hayo yataendelea kuwa changamoto katika hatua zote za ujenzi na kuleta taswira ya uharibifu katika hatua zote.

Changamoto zaidi ni kwamba jengo likishakosewa kwenye kusetiwa wakati wa kuseti msingi wa jengo sio rahisi tena kurekebisha kwani litahitaji kubomolewa lote na kuanza upya kabisa, kitu ambacho ni hasara kubwa kiasi kwamba sio rahisi kupata mtu wa kukubaliana nayo. Hivyo mtu anajukuta analazimika kuishi na makosa hayo ambayo tayari yalishafanyika tangu mwanzoni kwa kujitahidi kufukiafukia na kuishi nayo kama yalivyo.

Hivyo ni muhimu sana kabla ya ujenzi wa jengo lako kuanza kuhakikisha kwamba suala la kupatikana mraba wa jengo utakaomua mpangilio wa vipengele vya kwenye kwa hatua zote za ujenzi zinazofuata unazingatiwa, na zoezi hili litakuwa rahisi zaidi endapo atakuwepo msimamizi sahihi mwenye uzoefu wa kutosha katika kesi hiyo au apatikane mtu mwenye utaalamu wa masuala ya upimaji (surveyor).

Kwa kuzingatia hili unapata uhakika wa jengo lote kujengwa kwa usahihi tangu mwanzoni mpaka mwishoni na kila kitu kupangiliwa vizuri bila kuwepo kwa vitu vilivyokaa tenge ndani ya nyumba kama vile mpangilio wa makabati, vitanda, vigae vya sakafuni(tailizi) na mtiririko wa vitu vingine vyovyote.

Karibu sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *