DHANA YA UNAFUU WA GHARAMA KWENYE UJENZI.

Linapokuja suala la ujenzi nimekuwa nikiwashauri watu mbalimbali wanapoamua kujenga waanze kuweka mkazo kwanza kwenye kile wanachokitaka na wale wanayopendelea katika nyumba zao badala ya kuweka mkazo kwenye gharama za ujenzi. Ni kweli nafahamu kwamba gharama ndio mwamuzi mkuu lakini naamini kwamba kwa mtu yeyote kuna vipaumbele vyake ambavyo ni muhimu sana ambavyo havipaswi kuwekewa vikwazo na gharama kwa sababu ujenzi tu wenyewe kwa ujumla tayari ni gharama kubwa.

Changamoto kubwa ambayo huwa inatokea ni watu kuweka mkazo kwenye gharama na kuogopa sana gharama kiasi cha kuathiri maeneo muhimu lakini wakati huo huo bado utakuta hakuna mabadiliko makubwa sana wanayoweza kufanya kwenye kukwepa gharama hizo, kwa kiasi cha viwango vya wastani ambavyo nyumba husika inajengwa utakuta gharama haibadiliki kwa kiasi kikubwa sana.

Sababu kubwa ambayo huwa inapelekea watu wengi kupata hisia sana ni kuhusu gharama ni pamoja na kufikiri kwamba kwenye eneo la gharama kuna miujiza. Kwenye ishu ya gharama hakuna miujiza yoyote zaidi ni kwamba kwenye ishu ya gharama kuna maamuzi. Kwa sehemu kubwa kuongeza au kupunguza gharama ni suala la maamuzi binafsi, kwamba kama unahitaji kupunguza gharama basi ukubali kupunguza ukubwa wa nyumba ambao unatokana na kupunguza ukubwa wa vyumba ndani ya nyumba au idadi ya vyumba ndani ya nyumba.

Kitu kingine kinachopunguza gharama ni aina ya vifaa au hadhi ya vifaa vya ujenzi unavyoamua kuvitumia kwenye jengo lako hususan katika hatua ya umaliziaji(finishing), ambavyo mara nyingi hutofautiana sana gharama na mara nyingi utofauti huo husababishwa na ubora wa vifaa vyenyewe japo wakati mwingine huwa kuna sababu nyingine na haoo kwenye ubora ndio utakuta mara nyingi watu hawakubali kununua vya bei chini.

Mwisho wa siku utajikuta kwamba unaogopa sana gharama kwenye ujenzi na kujipa hofu kubwa sana katika eneo la gharama na kuishia kufanya maamuzi yasiyo sahihi kwako kutokana na kuongozwa na hisia halafu utajikuta hakuna kikubwa ulichokimbia lakini umeshindwa kuweka umakini maeneo muhimu na hivyo yakafanyika kwa namna ambayo unajikuta huifurahii baadaye.

Kupunuguza gharama na kujenga kwa unafuu hakuna miujiza wala hakuhitaji mtu kuwa na hofu sana bali kunahitaji maamuzi na mikakati, maamuzi ambayo kupungua huko kwa gharama pia kunaweza kuambatana na kukubali kupunguza vitu ambavyo sio vya lazima ndani ya jengo ambavyo pengine ungependa viwapo lakini ukaona ni gharama zisizo na lazima.

Hata hivyo kupunguza gharama kunahitaji kwanza uzifahamu gharama za ujenzi na matokeo ya gharama hizo kwanza kabla hujafikiri kama ni kubwa au ndogo. Watu wengi wamekuwa wakiogopa gharama sana lakini huku wakiwa hawajui hata gharama zenyewe ni kiasi gani, gharama yoyote wanayoambiwa wanaiona ni kubwa hata kama ni ndogo sana, hivyo ni muhimu kufahamu makadirio ya gharama ili uweze kujua kile haswa unachotaka kukipunguza na madhara yake.

Hivyo muhimu sana cha kwanza ni kujua unataka nini na kuweka mkazo katika kile unachokitaka kwanza kwa mfano unaweza kuwa unahitaji nyumba yenye faragha au yenye vyumba vikubwa kisha baada ya vipaumbele vyako hivyo ndipo unaanza kupunguza vile visivyokuwa muhimu.

Karibu sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *