WANAPOKUUZIA KIWANJA KWA UJENZI HALAFU WANATAKA HIFADHI KWENYE KIWANJA HICHO.

Imekuwa ikitokea kwa baadhi maeneo ambapo watu wamekuwa wakiuziwa kiwanja kwa ajili ya kukiendeleza maeneo mbalimbali halafu mara baada ya kuuza wale waliouza au ndugu zao wa karibu wanamwomba yule mmiliki aliyekinunua awape hifadhi waendelee kuishi eneo hilo mpaka pale atakapoamua kuanza mradi wake wa ujenzi au matumizi mengine yoyote ya kiwanja hicho ndipo waondoke wakatafute maeneo mengine ya kuishi.

Ombi la namna hiyo ni suala la kuwa nalo makini kwa sababu ni jambo ambalo limewagharimu na waliojikuta mwisho wa siku wanaishia kujuta kwa maamuzi yao ya kukubaliana nao. Kwa baadhi ya kesi za namna hii ambapo wakishaishi hapo kwa muda na kuona kwamba hawana uwezo wa kifedha wa kuhama na kutafuta sehemu nyingine ya kuishi huwa wanang’ang’ania eneo hilo moja kwa moja.

Huwa inatokea kwamba wanaweza kufoji nyaraka kwamba aidha eneo hilo ni la familia na limeuzwa kimakosa au wakaligawa kwamba eneo lako linaishia katikati kisha lililobaki ni eneo la familia na wakati mwingine kwa msaada wa majirani na viongozi wa eneo hilo wakapelekea kesi mahakamani kuzuia eneo ambalo wameamua kujipa kwamba ni haki yao.

Sasa pale wewe unapokuja na kuamua kwamba unataka kuanza kujenga eneo lako ndipo unakutana na changamoto kama hiyo ambayo hukuitegemea, watu ambao uliwaonea huruma na kuwapa hifadhi wamekugeuka na unashindwa kabisa kuamini imekuwaje, na kwa kuwa nao wanaona hawana pengine pa kwenda basi watapambana na wewe kwa hali na mali na saa nyingine hata kukuzidi nguvu au angalau kukupotezea mud asana.

Hivyo jambo la msingi sana unalotakiwa kuwa makini nalo ni kuweka umakini mkubwa sana pale unapokutana na ombi kama hilo na kama watu wenyewe ni wazoefu sana eneo hilo au wamezaliwa hapo na wewe huwafahamu kiundani ni afadhali ukatae ombi hilo kwa kuwaambia unataka kuanza kujenga baada ya siku chache sana pengine hata chini ya wiki moja na kwamba unahitaji waondoke eneo hilo mara moja na ikibidi ulizungushie kabisa uzio wa tofali au senyenge na kuweka geti kabisa.

Lakini pia ikiwa umeondoka halafu ukapata taarifa kwamba kuna watu wamehamia na wanaishi eneo lako pia ni muhimu sana kuwafuata na kuwaambia unaanza ujenzi mara moja n ahata ikiwezekana unaweza kupeleka kabisa mchanga eneo hilo na tofali kadhaa kuwaonyesha kwamba huwaondoi kwa sababu huwataki bali unataka kuanza ujenzi na hivyo unahitaji eneo libaki wazi.

Ni bora kuwa makini kiasi hicho mapema huruma yako isije ikakuponza kwa sababu wakishanogewa nae neo hilo na kuwamua kuanza kushughulika na wewe watakupotezea muda, usumbufu, gharama na pengine hata wakafanikiwa kukushinda pia. Hii ni changamoto ambayo tumeshakutana nayo mara kadhaa katika kazi zetu mbalimbali za ujenzi na inakuwa ni changamoto kiasi cha kusimamisha kabisa shughuli za ujenzi na kusababisha hata usumbufu na hasara kwetu na kwa mteja.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *