KUANGUKA KWA JENGO LA GHOROFA NI MATOKEO YA KUTOSHIRIKISHA UTAALAMU.

Najua watu wengi watasema kwamba hapana yapo majengo mengi wanashirikishwa wataalamu lakini bado yanaanguka. Hapa hakuna ukweli uliokamilika, ninapozungumza kushirikishwa utaalamu sizungumzii kushirikishwa utaalamu katika ngazi ya michoro peke yake na kusajili mradi, nazungumzia kushirikishwa utaalamu katika ngazi zote kuanzia wakati wa michoro ya ramani mpaka kwenye usimamizi wa jengo mpaka linakamilika.

Kwanza kabisa lazima tukubaliane kwamba kuanguka kwa jengo ni uzembe wa hali ya juu sana. Yaani kuanguka kwa jengo hakusababishwi tu na kukosekana kwa mtaalamu peke yake bali kunasababishwa pia na maamuzi ya mradi kuachwa kwa mafundi ambao hawana uelewa na uzoefu wa kusimamia majengo ya ukubwa huo.

Inafahamika wazi kwamba jengo la ghorofa linahitaji michoro ya aina mbili ambayo ni ile michoro ya usanifu wa jengo sambamba na michoro ya uhandisi mihimili ya jengo lenyewe. Michoro ya usanifu wa jengo ndio michoro haswa ya jengo lenyewe. Kisha michoro ya uhandisi mihimili ni inayoonyesha mpangilio wa vyuma na zege ambalo ndilo linalohakikisha uimara wa jengo husika.

Sasa mtaalamu anayefanya kazi ya kutengeneza michoro ya uhandisi mihimili ni mtaalamu aliyebobea kiasi kwamba michoro hiyo huwa inatengenezwa kwa namna ambayo itamudu kubeba mzigo wa jengo husika akitumia taaluma na uzoefu ambazo ni “basic skills” za kawaida kabisa katika taaluma ya uhandisi. Ambapo ikiwa jengo lilihusisha michoro ya uhandisi mihimili ni wazi kwamba kama michoro hiyo ikifuatwa kadiri ya mapendekezo ya kitaalamu mzigo husika unabebwa vizuri bila shida.

Changamoto inakuja pale ambapo watu wenye dhamana katika ujenzi wa mradi huo aidha wanapopuuzia mapendekezo ya kitaalamu na kufanya wanavyotaka wao au wanapoamua kuchakachua ili waweze kupunguza gharama au kupata faida zaidi katika mradi husika. Watu hawa wanaweza kuwa aidha ni mafundi waliopewa dhamana au mteja mwenyewe mwenye jengo akiwasikiliza watu ambao wanajaribu kumpotosha ili kumfurahisha.

Lakini kwa mtaalamu ambaye anaelewa vizuri kile kinachofanyika na kufahamu matokeo ya majanga ambayo yatakuja mbeleni kutokana mambo wanayojaribu kufanya kamwe hawezi kuruhusi uchakachuaji wa namna hiyo. Hii ni sawa dereva anayejua kabisa kwamba gari haina breki halafu unamwambia aendeshe kwa kasi kuelekea kwenye mteremko ambapo anaenda kufikia kwenye makazi ya watu, ni wazi kwamba kamwe hawezi kukubaliana na hilo kwa sababu anafahamu matokeo yake.

Hivyo inawezekana kabisa mradi ukahusisha wataalamu katika hatua ya michoro kisha kazi ya kujenga ikaachwa kwa watu wasio na utaalamu wala uzoefu mkubwa, kisha kwa tamaa au kutokujua wakaamua kuchakachua au kushindwa kuelewa vizuri nini cha kufanya na kupelekea jengo kukosa uimara na kuanguka.

Hivyo tunaendelea kusisitiza kwamba, ili kuepuka changamoto za udhaifu wa jengo ambapo kuna mengine hayaanguki mara moja lakini yanakuwa na maisha mafupi kutokana na kiwango cha uchakachuaji kilichofanyaika. Kwa maana hiyo ni muhimu sana kushirikisha utaalamu katika hatua zote za ujenzi kuanzia kwenye ngazi ya kuandaa michoro ya ramani mpaka kwenye usimamizi na ukaguzi wa mradi husika kuhakikisha kwamba kila kitu kinafuata maelekezo yote ya kitaalamu yaliyopendekezwa kwenye michoro na hata wakati wa ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *