HATUA MUHIMU KATIKA UJENZI AMBAZO NI LAZIMA KUHUSISHA UTAALAMU.

Licha ya kwamba tunahimiza sana umuhimu wa mradi mzima wa ujenzi kutumia utaalamu kuanzia mwanzo mpaka mwisho ili kuzingatia ubora na kanuni sahihi za kitaalamu katika ujenzi lakini kuna maeneo ambayo ni muhimu zaidi angalau yasimamiwe, kukaguliwa na kuhakikiwa na mtaalamu kwa sababu ndio maeneo ambayo ni rahisi kufanyika makosa, na mara makosa yanapofanyika kuja kurekebisha ni kazi ngumu na ya gharama kubwa sana na wakati mwingine inaweza kushindikana kabisa pia.

Kuna maeneo manne au matano ambayo ni muhimu sana katika ujenzi kuhakikisha kwamba yanasimamiwa na kukaguliwa na mtaalamu ili kuhakikisha makosa kwenye jengo yanapungua kwa kiasi kikubwa na hata ambayo yatakuwepo basi hayatakuwa makosa makubwa sana ya kiufundi, bali ni ambayo yanawezekana kurekebishika na mara nyingi hayatumii gharama kubwa sana.

Moja ya maeneo haya ni kwenye hatua ya kutengeneza michoro ya ramani ya jengo. Katika kutengeneza michoro ya ramani ya jengo hapo ni muhimu sana kumhusisha mtaalamu kwani ramani ya jengo ndio msingi wa mahitaji yako na ndio mwongozo wa ujenzi mzima. Ni kosa kubwa sana la kiufundi kutomhusisha mtaalamu wa kutengeneza michoro ya ramani katika hatua ya mwanzo kabisa kwani unajiandaa na kazi mbovu ya viwango duni na ambayo pengine utaijutia maisha yako yote. Kitu muhimu zaidi ambacho mtaalamu wa kutengeneza michoro ya ramani ya jengo atakachokusaidia ni kuhakikisha unapata kile hasa unachokitaka wewe na sio kuiga wengine ambao wana mahitaji yasiyoendana na ya kwako sambamba na kuhakikisha mahitaji yako unayapata yaliyozingatia utaalamu wa viwango bora. Hatua ya kutengeneza michoro ya ramani ndio hatua muhimu zaidi ya kumhusisha mtaalamu kuliko hatua nyingine yoyote.

Mbili ni wakati wa kuleseti jengo katika eneo husika na katika uelekeo husika sambamba na kuhakikisha vyote muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa katika hatua ya msingi vinakuwepo. Hatua hii ya kuseti msingi wa jengo ni muhimu sana kwa sababu inapokosewa inasababisha jengo zima kukosea kuanzia uimara wa msingi wenyewe mpaka sehemu sahihi ya kuuseti msingi huo. Hatua hii ya kuseti msingi wa jengo pia ndio huamua mpangilio wa vyumba ndani ya jengo kwa sakafu ya chini kabisa katika jengo ambayo pia mara nyingi ndio msingi wa uimara wa mfumo mzima wa mihimili ya jengo husika.

Tatu ni ukaguza wa vipengele vya jengo vya wima na ulalo katika kuta kuhakikisha kwamba vimefanyika kwa kuzingatia usahihi wa vipimo na mipangilio kwa sababu vina umuhimu mkubwa sana kiufundi na hata katika kuamua ubora wa muonekano wa jengo. Katika hatua hii mtaalamu anaweza kuwa kwenye nafasi ya kufanya ukaguzi zaidi na kupendekeza maeneo ambayo ni muhimu yakafanyiwa marekebisho baada ya kufanya makosa. Hatua hii kwa sehemu kubwa makosa yake huweza kurekebishika japo wakati mwingine kwa gharama kubwa sana, lakini yasiporekebishwa huchangia sana kuharibu sura ya jengo na hata wakati mwingine kuchangia baadhi ya kero za jengo husika kiufundi.

Nne ni paa la jengo. Hili huchangia sana muonekano wa jengo na linapofanyika katika viwango visivyosahihi husababisha muonekano wa hovyo sana wa jengo. Paa pia linaposhindwa kufanyika kwa usahihi huweza kuwa chanzo cha kero nyingi sana katika jengo kama vile maji kuvujia ndani ya nyumba au kumwagika hovyo na kusababisha changamoto nyingine nje ya nyumba.

Tano ni zile sakafu za ghorofa za juu zaidi kwa majengo ambayo ni ya ghorofa. Kiufundi kabla ya kumimina zege la sakafu za juu za jengo ni muhimu taarifa zote zikakaguliwa kitaalamu kuhakikisha kwamba kila kitu kimefanyika kwa usahihi kwa sababu madhara yake kazi ya hovyo katika hatua hii ni nyeti na makubwa. Muhimu pia katika hatua hii ni kukaguwa mpangilio wa kuta za sakafu husika kama zimefanyika kwa usahihi kuanzia mpangilio wake wa vyumba mpaka mpangilio wima unaohakikisha mfumo wa mihimili wa jengo umepangiliwa kwa usahihi.

Hizo ndio hatua zile kubwa na muhimu ambazo mtaalamu hatakiwi kukosa kuwa amezikagua kwa sababu madhara yanayosababishwa na makosa yake huwa kwa kawaida ni makubwa sana na yanahusisha gharama kubwa sana kuyarekebisha au mengine hayarekebishiki kabisa.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *