TATIZO LA KWENYE UJENZI NI KWAMBA UTAJUA HUJUI KWA KUCHELEWA.

Mara kwa mara nimekuwa nikisisitiza kwamba hakuna kitu cha muhimu kuzingatia kama ubora wa utaalamu unaoenda kutumika kwenye mradi wa ujenzi. Lakini changamoto za watu kupuuza huduma bora za kitaalamu bado ni tatizo kubwa. Hii ni kwa sababu watu wengi hujidanganya kwamba wanajua na vitu vingi vinaeleweka lakini katika uhalisia kuna vitu vingi sana ambavyo watu hawajui na mbaya zaidi ni kwamba hawakijui kile wasichokijua. Baadaye ndio huja kujua kwamba hawajui wakati mambo yameshaharibika.

Ujenzi una mambo mengi sana, na watu ambao angalau wanaweza kuepuka makosa kwa kiasi kikubwa ni wale wabobezi ambao wameshafanya kazi kwa muda mrefu sana katika miradi inayofanyika kwa umakini kabisa na inayosimamiwa na wataalamu katika hatua muhimu. Tofauti nah apo makosa ni mengi sana ambayo hujitokeza kila siku na kuharibu kazi. Kwa mfano siku za hivi karibuni kuna mteja aliondoka na michoro akasema bado hajaanza kazi, lakini akaweza kupata fundi mwingine huko wakaanza kazi ya kuseti na kuanza kuchimba msingi bila kutoa taarifa yoyote.

Baadaye tunafika tunakuta wanakaribia kukamilisha msingi wa jengo uliowagharimu zaidi ya milioni 30 lakini wamekosea namna ya kuweka uelekeo wa jengo. Fikiria ni jengo la milioni kama 600 lakini linakosewa kuwekwa uelekeo na mvuto wake kupungua kwa sababu ya kushindwa kumshirkisha mtaalamu ambaye asingegharimu hata zaidi ya shilingi laki moja. Huu ni mfano mdogo tu wa makosa madogo dogo lakini watu wengi wamekuwa wanatumia gharama kubwa katika vifaa vya ujenzi na kushindwa kuweka wataalamu au mafundi wenye uwezo na kuishia kuchelewesha mradi na hata kufanya kazi ya viwango duni kwa kufikiri wanajua kumbe hawajui kile wasichojua na hivyo wanakuja kujua kwamba hawajui wakati wameshachelewa. Changamoto nyingi na makosa mengi sio rahisi kuonekana katika nadharia ni mpaka uingie kwenye vitendo ndio utagundua jinsi kuna utata mkubwa.

Suala la ufundi bora au kuzingatia utaalamu ni jambo muhimu sana pengine kuliko hata kukimbilia kununua vifaa vya bei ambavyo vitakuja kuishia kufanyika kwa viwango duni.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *